• HABARI MPYA

  Sunday, August 06, 2017

  KIPIGO CHA YANGA JANA, SINGIDA UNITED ‘YABOMOA’ USAJILI, YALETA MSHAMBULIAJI WA KAIZER CHIEFS

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KUFUATIA kipigo cha mabao 3-2 jana kutoka kwa Yanga, kocha wa Singida United, Mholanzi Hans van der Pluijm amerudi nyuma na kurekebisha kidogo usajili wake. 
  Timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, imemchukua mshambuliaji Michelle Katsavairo kutoka klabu ya Keizer Chiefs ya Afrika Kusini na kumuacha Mzimbabwe mwenzake, Wisdom Mtasa.
  Mkurugenzi wa Singida United, Sanga Festo amesema kwamba baada ya kusajiliwa kwa Katsavairo kutoka Kaizer, Mtasa anapalekwa kwa mkopo wa Stand United ya Shinyanga.
  Kocha wa Singida United, Mholanzi Hans van der Pluijm amerekebisha kidogo usajili wake baada ya kipigo cha Yanga jana 

  Sanga amesema kwamba wamefanya hivyo ili kupata nafasi ya kusajili mchezaji mwingine wa kigeni kwa mujibu wa kanuni, ambayo inataka kila klabu kusajili wageni saba tu. 
  Wachezaji wengine wa kigeni Singida United baada ya kuondoka kwa Mtasa ni Simbarashe Nhivi, Danny Usengimana, Michael Rusheshangoga (Rwanda), Tafadwaza Kutinyu na Simbarashe Nhivi wote kutoka Zimbabwe na Shafik Batambuza wa Uganda.
  Singida United jana imefungwa mabao 3-2 na Yanga licha ya kuongoza kwa mabao 2-1 hadi mapumziko, mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Shujaa wa Yanga katika mchezo wa leo alikuwa ni kiungo mshambuliaji, Emmanuel Martin aliyefunga bao la ushindi kwa shuti la umbali wa mita 23 baada ya pasi ya mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe.
  Singida walikwenda kupumzika wakiwa wanaongoza kwa 2-1, mabao yote matatu yakifungwa na wachezaji wa kigeni kipindi cha kwanza.
  Kiungo Mzimbabwe, Thabani Scara Kamusoko alianza kuifungia Yanga bao la kwanza dakika ya tano kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya mshambuliaji mpya, Ibrahim Hajib kuangushwa umbali wa mita 25.
  Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Azam Rwanda kwa misimu yote miwili iliyopita, Dany Usengimana akaifungia Singida United bao la kusawazisha dakika ya nane akitumia vizuri makosa ya nabeki wa Yanga kuchanganyana.
  Michelle Katsavairo kutoka Keizer Chiefs amechukua nafasi ya Mzimbabwe mwenzake, Wisdom Mtasa ndani ya Singida United

  Mshambuliaji Mzimbabwe, Simbarashe ‘Simba’ Nhivi Sithole akaifungia bao la pili Singida dakika ya 23 akitumia tena makosa ya safu ya ulinzi ya Yanga.
  Kipindi cha pili, kocha Mzambia wa Yanga alibadilisha karibu kikosi kizima akimtoa hadi kipa Beno Kakolanya na kumuingiza Mcameroon, Yoouth Rostand.
  Mabadliko hayo yaliisaidia Yanga kupata mabao mawili dakika za mwishoni, akianza Mrundi Tambwe kusawazisha kwa penalti dakika ya 83 baada ya kipa Said Lubawa kumchezea rafu kiungo chipukizi, Said Juma, kabla ya Emmanuel Martin kufunga la ushindi dakika yab 90 na ushei.
  Katika mchezo huo, Singida walipoteza mikwaju miwili ya penalti, wa kwanza dakika ya kwanza kabisa Elisha Muroiwa akipaisha juu ya lango na ya pili, kipa Rostand akiokoa shuti la pembeni la mshambuliaji Atupele Green.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIPIGO CHA YANGA JANA, SINGIDA UNITED ‘YABOMOA’ USAJILI, YALETA MSHAMBULIAJI WA KAIZER CHIEFS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top