• HABARI MPYA

  Saturday, August 12, 2017

  MKUTANO WA SIMBA KUMKABIDHI RASMI TIMU MO DEWJI KUFANYIKA JUMAPILI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Simba imewataka wanachama wake kujitokeza kwa wingi katika Mkutano wake mkuu wa kawaida wa kila mwaka utakaofanyika Jumapili kuanzia Saa 4:00 asubuhi kwenye Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere (MNICC).
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Sunday Manara amesema kwamba Mkutano wa Jumapili upo pale pale baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kutupilia mbali ombi la mmoja wa Wadhamini wa klabu hiyo, Mzee Hamisi Kilomoni kuzuia mkutano huo.
  “Ukumbi huo wa kisasa kabisa nchini upo maeneo ya Ocean Road, jirani na Chuo cha Usimamizi wa fedha (IFM) na itakuwa mara ya kwanza kwa klabu ya michezo nchini kufanyia mkutano wake kwenye kituo hicho kilichobeba jina la Baba wa Taifa hili,”amesema Manara na kuongeza;
  “Uongozi wa Simba unawaomba wanachama wake kuhudhuria kwa wingi kwenye mkutano huo muhimu, huku mahitaji yote muhimu yakipatikana siku hiyo ikiwemo vinywaji baridi na chakula cha mchana,”.
  Mohammed Dewji anataka kuuziwa asilimia 51 ya hisa za Simba kwa Sh. Bilioni 20  

  Manara amesema uamuzi wa Mahakama ni ushindi mkubwa siyo tu kwa klabu, bali kwa mustakbali mzima wa maendeleo ya mchezo wa soka nchini, kote.
  Wazi mkutano huo unakwenda kupitisha uamuzi wa kumuuzia hisa mfadhili wa klabu hiyo, Mohammed Dewji awe mmiliki rasmi wa Simba.
  Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini anataka kuuziwa asilimia 51 ya hisa za klabu kwa Sh. Bilioni 20 na baada ya hapo atatumia bajeti ya Sh. Bilioni 5.5 kwa msimu kwa ajili ya Simba SC, ili kuwapiku wapinzani Azam na Yanga.
  Na Rais huyo wa Kapuni ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL) amesema akiuziwa asilimia 51 ya hisa na kuwa mmiliki wa Simba, atawawezesha wanachama wa muda mrefu wa klabu hiyo kupewa hisa bure, ambazo wataamua wenyewe kuuza, au kununua hisa zaidi. 
  Na o ofa hiyo ya tajiri huyo kijana zaidi Afrika kwa mujibu wa jarida la Forbes, anataka kuweka Bilioni 1.5 kila mwaka ili kukamilisha ujenzi wa Uwanja ndani ya miaka mitatu ambao utakuwa wa kisasa utakaotupa fursa ya kuanzisha na miradi ya soka ya vijana. 
  Amesema lengo lake ni kuifanya Simba itwae ubingwa wa Afrika kwa kushindana na timu kama TP Mazembe zinazotumia Bajeti ya Sh. Bilioni 20 kwa mwaka.
  Mo Dewji (kushoto) anataka kutumia Sh. Bilioni 5 kuijengea Simba Uwanja wa kisasa ndani ya miaka mitatu

  Mo Dewji amesema kwa kuwa Simba ina majengo pacha mawili Mtaa wa Msimbazi na kiwanja wa Bunju, atatumia Sh. Bilioni 5 kujenga Uwanja wa kisasa ndani ya miaka mitatu.
  Mo Dewji ni mpenzi na mwanachama wa Simba SC, ambaye kati ya 1999 na 2005 alikuwa mdhamini Mkuu wa klabu na akazishawishi pia Simba Cement na NBC kuwekeza katika klabu hiyo hadi ikafuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 ikiitoa Zamalek ya Misri.
  Mo pia amewahi kuwa mdhamini wa Singida United na mmiliki wa African Lyon kwa muda, kabla ya kuiuza kwa mfanyabishara Rahim ‘Zamunda’ Kangenzi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MKUTANO WA SIMBA KUMKABIDHI RASMI TIMU MO DEWJI KUFANYIKA JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top