• HABARI MPYA

  Thursday, August 10, 2017

  BEKI MNIGERIA AVUTIA KWENYE MAJARIBIO YANGA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI wa kati Mnigeria, Kehinde ‘Kenny’ Yisa Anifowoshe maarufu tu kama Yisa Anifowoshe  (pichani kulia) yuko kwenye nafasi nzuri ya kusajiliwa Yanga SC baada ya kuvutia katika majaribio.
  Mchezaji huyo ambaye Oktoba 11, mwaka huu atafikisha umri wa miaka 25, msimu uliopita alichezea Al Ittihad SC ya Oman kuanzia Januari mwaka huu na amekuja Tanzania kujaribu kubadilisha upepo baada ya kucheza Afrka Magharibi na Asia.
  Na katika mazoezi ya leo, Anifowoshe alionekana kucheza vizuri na kumvutia kocha Mzambia, George Lwandamina ambaye anasubiriwa kutoa uamuzi ili asajiliwe.
  Yanga ina nafasi moja ya kusajili mchezaji wa kigeni na na inataka zaidi kuchukua beki wa kati kuziba pengo la Mtogo, Vincent Bossou, kwani tayari Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi ameziba pengo la Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.
  Kuna uwezekano mkubwa Anifowoshe aliyewahi kuchezea MFM FC ya kwao akapewa nafasi ya kucheza Jumamosi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Huo utakuwa mchezo wa pili rasmi wa kujipima nguvu kwa Yanga, baada ya Jumamosi iliyopita kuifunga Singida United mabao 3-2 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.  
  Lakini utakuwa mchezo wa kwanza baada ya Yanga kukamilisha usajili wake wa msimu mpya- maana yake huo ndio mchezo ambao mashabiki wa timu hiyo watapata fursa ya kukijua rasmi kikosi chao kamili cha msimu mpya.
  Yisa Anifowoshe wakati anasajiliwa Al Ittihad SC ya Oman Januari mwaka huu

  Kwa kocha Lwandamina huo utakuwa mchezo wa kukipima kikosi chake kwa mara ya mwisho kabla ya kuingia kwenye mchezo na wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu, Simba Agosti 23 Uwanja wa Taifa.
  Lwandamina bila shaka Jumamosi atampanga pia Tshishimbi kwa mara ya kwanza baada ya kusajiliwa kutoka Mbabane Swallows ya Swaziland. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BEKI MNIGERIA AVUTIA KWENYE MAJARIBIO YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top