• HABARI MPYA

  Friday, August 11, 2017

  YANGA NA RUVU SHOOTING SASA KUCHEZWA CHAMAZI KESHO JIONI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM 
  SERIKALI imeizuia klabu ya Yanga kuutumia Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kwa mechi ya kirafiki Jumamosi kwa kile kilichoelezwa kupisha shughuli maalum wikiendi hii.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani mjini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba sasa mchezo wao na Ruvu Shooting utafanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  "Kwa sababu hiyo mchezo wetu wa kirafiki na Ruvu Shooting uliokuwa ufanyike Uwanja wa Taifa unahamia Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kama kawaida Jumamosi Saa 10:00 jioni,"amesema Mkwasa.


  Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina (katikati) akiwa na wasaidizi wake, Noel Mwandila na Nsajigwa Shadrack (kushoto)

  Huo utakuwa mchezo wa pili rasmi wa kujipima nguvu kwa Yanga, baada ya Jumamosi iliyopita kuifunga Singida United mabao 3-2 Uwanja wa Taifa.  
  Lakini utakuwa mchezo wa kwanza baada ya Yanga kukamilisha usajili wake wa msimu mpya- maana yake huo ndio mchezo ambao mashabiki wa timu hiyo watapata fursa ya kukijua rasmi kikosi chao kamili cha msimu mpya.
  Kwa kocha Mzambia, George Lwandamina huo utakuwa mchezo wa kukipima kikosi chake kwa mara ya mwisho kabla ya kuingia kwenye mchezo na wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu, Simba Agosti 23 Uwanja wa Taifa.
  Lwandamina bila shaka Jumamosi atampanga pia Tshishimbi kwa mara ya kwanza baada ya kusajiliwa kutoka Mbabane Swallows ya Swaziland. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA NA RUVU SHOOTING SASA KUCHEZWA CHAMAZI KESHO JIONI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top