• HABARI MPYA

  Monday, August 14, 2017

  JUUKO AREJEA SIMBA BAADA YA KUFELI MAJARIBIO ORLANDO PIRATES

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI wa kati Mganda, Juuko Murshid amerejea katika klabu yake, Simba SC baada ya kufeli majaribio klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba Murshid aliyezaliwa Aprili 14, mwaka 1994 amewasili Dar es Salaam leo na kesho atakwenda Zanzibar kuungana na wachezaji wenzake kambini.
  “Napenda kuchukua nafasi hii kuwaondoa wasiwasi wapenzi na wanachama wa Simba kuhusu Juuko ambaye ilikuwa inaelezwa atakwenda kwa wapinzani wetu kwa kuwaambia kwamba Juuko amerudi na kesho anakwenda kambini Zanzibar,”amesema Hans Poppe.
  Zacharia Hans Poppe (kulia) akiwa na Juuko Murshid leo baada ya kurejea nchini
  Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba Juuko alipewa ruhusa maalum kubaki Afrika Kusini baada ya kambi ya wiki mbili ya Simba nchini humo, ili afanye majaribio Orlando Pirates, lakini bahati mbaya hakufanikiwa na amerudi.
  Kocha kipenzi wa Juuko, Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ alipenda kuendelea kufanya kazi na beki huyo wa kati baada ya kuachana na timu ya taifa ya Uganda na kuhamia Ligi Kuu ya Afrika Kusini, lakini bahati mbaya mpango huo umeshindikana kwa sasa.
  Na sasa Juuko atavuka bahari kwenda kuungana na kikosi cha Simba kwa maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu, Yanga Agosti 23, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: JUUKO AREJEA SIMBA BAADA YA KUFELI MAJARIBIO ORLANDO PIRATES Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top