• HABARI MPYA

  Saturday, August 05, 2017

  AZAM YAAMUA KUMUACHIA GARDIEL AENDE YANGA ‘KIROHO SAFI’

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  BAADA ya mavutano ya hapa na pale, hatimaye Yanga na Azam FC wamefikia makuabaliano mazuri juu ya beki chipukizi wa kushoto, Gardiel Michael Mbaga.
  Beki huyo wa kimataifa wa Tanzania anahitimisha maisha yake ya kichezaji ndani ya Azam FC yaliyoanzia tangu akademi ya klabu hiyo yenye maskani yake Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na kuhamia Yanga SC.
  Gardiel amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC na bahati nzuri, klabu yake Azam FC imeridhia aondoke, japokuwa mkataba wake unamalizika Desemba.  
  Yanga SC imemtambulisha rasmi Gardiel Michael leo baada ya kumalizana Yanga

  Taarifa ya Azam FC leo imesema; “Kwa muda mrefu Yanga imekuwa ikionyesha nia ya kumsajili beki huyo, lakini haikuwahi kuja kufanya mazungumzo kwa ajili ya kuuvunja mkataba wake unaomalizika Desemba mwaka huu,”.
  “Tunashukuru viongozi wa Yanga wamekuwa waungwana na kuamua kufika leo kwenye ofisi zetu wakiongozwa na Mwenyekiti wa Usajili, Hussein Nyika, na hatimaye baada ya mazungumzo tukafikia muafaka kwenye suala hilo,”.
  “Hivyo baada ya pande zote kukubaliana ni rasmi sasa, tunathibitisha ni ruksa kwa Yanga kumsajili Gadiel kwa msimu ujao na tunamtakia kila la kheri katika maisha yake mapya ndani ya timu hiyo,”.
  “Azam FC ni timu inayoendeshwa kiueledi haiwezi kumbania mchezaji yoyote kuondoka kusaka malisho bora kama taratibu za usajili zimefuatwa,” imesema taarifa hiyo katika tovuti rasmi ya Azam.
  Na baadaye, Yanga kupitia akaunti yao ya Instagram wakatangaza kumsajili mchezaji huyo kwa mkataba wa miaka miwili. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM YAAMUA KUMUACHIA GARDIEL AENDE YANGA ‘KIROHO SAFI’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top