• HABARI MPYA

    Wednesday, September 03, 2014

    YANGA SC: VIONGOZI SIMBA NI WAPENDA SIFA NA WENYE KUWAHADAA WANACHAMA WAO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MAKAMU Mwenyekiti wa Yanga SC, Clement Sanga amesema kwamba viongozi wa Simba wanafanya kazi kwa kupenda sifa na kuwahadaa wanachama wao, ndiyo maana wakamsajili Emmanuel Okwi.
    “Tatizo lililopo Simba kwa sasa ni tabia ya viongozi wa klabu hiyo kupenda sifa. Wameamua kumsajili Okwi ili kuwafurahisha wanachama na mashabiki wa klabu yao,” amesema Sanga akizungumza na BIN ZUBEIRY leo.
    Sanga amesema kwamba Yanga haina cha kupoteza kwa Mganda huyo aliyetimkia kwa watani wao hao wa jadi, Simba.
    Okwi, aliyejiunga na Yanga siku ya mwisho ya usajili wa dirisha dogo Desemba 15, mwaka jana, kwa mkataba uliodaiwa kuwa wa miaka miwili na nusu, alijiunga na Simba Alhamisi iliyopita na kuzua mjadala mkubwa nchini.
    Wakati hatma ya mshambuliaji huyo wa zamani wa SC Villa ya Uganda na Etoile du Sahel ya Tunisia ikitarajiwa kujulikana Jumamosi baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF kukutana, uongozi wa Yanga umesema hauna cha kupoteza kwa kuwa hakuwa kwenye mipango yao ya msimu huu.
    Makamu Mwenyekiti wa Yanga SC, Clement Sanga kushoto amesema viongozi wa Simba SC wanapenda sifa

    Sanga ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba klabu hiyo ya Jangwani haina hasara kumkosa mchezaji huyo kwa kuwa alikuwa miongoni mwa wachezaji wao waliokuwa katika orodha ya kutemwa.
    “Yanga hatuna hasara ya kumkosa Okwi, hakuwa katika mipango ya msimu huu na ni miongoni mwa wachezaji ambao tulikuwa tumepanga kuwatema,” amesema Sanga.
    Alipoulizwa kwa nini wamemshtaki mchezaji huyo baada ya kuripotiwa kujiunga na Simba, Sanga amesema: “Njia alizozitumia kujiunga na Simba si sahihi kwa sababu bado alikuwa hajamalizana na Yanga. Sisi tuna madai yetu, naye ana yake lakini amekiuka taratibu za kimkataba na kisoka kwa kuzungumza na Simba na klabu nyingine kwa nia ya kusajiliwa.”
    Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zinadai kuwa kocha mpya wa mabingwa hao mara 24 wa Ligi Kuu nchini, Mbrazil Marcio Maximo ndiye aliyeharibu hali ya hewa kwa Okwi baada ya kuuagiza uongozi wa klabu hiyo kusitisha mkataba wake baada ya kupata taarifa juu ya utukutu wake.
    Chanzo chetu kinadai kuwa katika kikao cha kocha huyo na uongozi wa juu wa klabu kuamua mchezaji yupi aondoke kati ya Genilson Santana Santos 'Jaja' na Okwi, Maximo aliutaka uongozi usitishe mkataba wa Okwi.
    “Maximo alikataa pendekezo la uongozi kusitisha mkataba wa Jaja na akawa amepanga kuachia ngazi kuifundisha timu kama pendekezo lake lingelikataliwa,” kimeeleza chanzo chetu.
    Okwi, aliyekosa mechi kadhaa za mwanzoni mwa msimu uliopita wa VPL baada ya kuzuiwa na TFF kabla ya kugoma kuichezea Yanga katika mechi nne za mwishoni mwa msimu huo akidai kutolipwa sehemu ya pesa za usajili wake katika klabu hiyo, amekuwa katika msuguano na klabu zinazomsajili tangu aondoke Simba Januari mwaka jana na kujiunga na Etoile du Sahel ya Ligi Kuu ya Tunisia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC: VIONGOZI SIMBA NI WAPENDA SIFA NA WENYE KUWAHADAA WANACHAMA WAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top