• HABARI MPYA

    Thursday, September 25, 2014

    SIMBA NA YANGA YAAHIRISHWA, TAREHE MPYA KUTAJWA KESHO…WAPISHA MTANANGE WA STARS NA BENIN TAIFA OKTOBA 12

    Na Dina Ismail, DAR ES SALAAM
    MECHI ya watani wa jadi, Simba SC na Yanga SC mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara iliyokuwa ichezwe Oktoba 12, mwaka huu imefutwa na sasa tarehe mpya itatajwa kesho.
    Taarifa ya TFF leo imesema kwamba, hiyo iantokana na mchezo wa kirafiki wa kimataifa baina ya Taifa Stars na Benin ambao kwa ujumla utabadilisha ratiba ya Ligi Kuu na marekebisho hayo yatatangazwa kesho (Septemba 26 mwaka huu).
    Taifa Stars inashuka uwanjani Oktoba 12 mwaka huu kuikabili Benin katika mechi ya kirafiki ya kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
    Mechi ya Stars na Benin imeahirisha pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga SC Oktoba 12 mwaka huu

    Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Programu ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kwa ajili ya mechi hiyo itatangazwa baadaye na Kocha Mkuu Mart Nooij.
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linaendelea na taratibu nyingine kwa ajili ya mechi hiyo ikiwemo usafiri wa Benin kuja nchini, ambapo timu hiyo inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Oktoba 10 mwaka huu ikiwa na msafara wa watu 28.
    Pambano la Stars na Benin litatanguliwa na mechi ya kudumisha upendo kati ya viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu.
    Wakati huo huo: Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi anatarajia kufunga mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa vyama vya mpira wa miguu wa wanawake vya mikoa ya Tanzania Bara.
    Hafla ya kufunga mafunzo hayo itafanyika kesho (Septemba 26 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF, Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
    Mafunzo hayo ya siku tano yalishirikisha viongozi 34 wakiwemo baadhi ya waandishi wa habari na Meneja wa Twiga Stars, na yaliendeshwa na Mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Henry Tandau.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NA YANGA YAAHIRISHWA, TAREHE MPYA KUTAJWA KESHO…WAPISHA MTANANGE WA STARS NA BENIN TAIFA OKTOBA 12 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top