• HABARI MPYA

    Wednesday, September 03, 2014

    TFF YASOGEZA MBELE MCHEZO WA NGAO YANGA NA AZAM FC, SASA UTAPIGWA JUMAPILI TAIFA

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeusogeza mbele kwa siku moja, mchezo wa Ngao ya Jamii baina ya mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Azam FC dhidi ya washindi wa pili, Yanga SC.
    Sasa mchezo huo, uliokuwa ufanyika Septemba 13, mwaka huu utafanyika Septemba 14 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia Saa 10:00 jioni. 
    Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba wamechagua Jumapili kwa sababu ni siku ambayo tulivu zaidi, hivyo watu wengi watapata fursa ya kwenda uwanjani. 
    Mrisho Ngassa wa Yanga SC akikimbizana na David Mwantika wa Azam katika mchezo wa Ligi Kuu msimu uliopita. Wachezaji hao wanatarajiwa kukutana tena Jumapili wiki ijayo

    “Mchezo wa mwaka huu utaambatana na shughuli za kijamii kama uchangiaji damu na maonyesho ya shughuli za wadau na maendeleo ya jamii. TFF itatoa sehemu ya mapato ya mchezo huu kuchangia shughuli ya kijamii iliyochaguliwa,”amesema Mwesigwa
    Mchezo huo wa kuashiria kupenuliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, utakuja wiki moja kabla ya kitimutimu cha ligi hiyo kuanza. 
    Ligi Kuu inatarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu, mabingwa watetezi, Azam FC wakifungua dimba na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Septemba 20, mwaka huu, wakati Yanga SC waliomaliza nafasi ya pili wataanza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro siku hiyo.
    Washindi wa tatu, Mbeya City wataanza na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Sokoine, Mbeya Septemba 20 na washindi wa nne Simba SC watafungua dimba na Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Septemba 21.
    Mechi nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu zitakuwa kati ya Stand United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YASOGEZA MBELE MCHEZO WA NGAO YANGA NA AZAM FC, SASA UTAPIGWA JUMAPILI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top