• HABARI MPYA

    Friday, September 26, 2014

    UCHAGUZI MKUU ZFA JANUARI 3

    Na Ameir Khalid, ZANZIBAR
    UCHAGUZI Mkuu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), unatarajiwa kufanyika Januari 3, 2015 katika sehemu itakayotajwa baadae.
    Mkutano Mkuu wa chama hicho utakaofuatiwa na uchaguzi huo, umepangwa kufanyika baada ya kukamilika taratibu za uchaguzi wa ngazi ya wilaya pamoja na kamati za kudumu za chama hicho, zinazotarajiwa kuanza Oktoba 25 mwaka huu.
    Katika mkutano na waandishi wa habari jana, Rais wa ZFA Ravia Idarous Faina alisema,  chama chake kimeamua kutoa taarifa ya utaratibu wa chaguzi hizo mapema ili kuepuka mgogoro wa kikatiba.
    Rais wa ZFA, Ravia Idarous akihutubia katika moja ya hafla za chama hicho

    Alisema taratibu za uchaguzi ngazi ya wilaya na kamati za kudumu za chama hicho, zinatakiwa kumalizika Disemba 27 mwaka huu, kutoa nafasi kwa harakati za uchaguzi mkuu kuanza rasmi.
    Rais huyo aliyeingia madarakani Juni 8, 2013 kufuatia uchaguzi mdogo uliofanyika baada ya kujiuzulu kwa Amani Ibrahim Makungu.
    Makungu pia alishika wadhifa huo kwa uchaguzi mdogo baada ya kuachia ngazi aliyekuwa Rais kwa zaidi ya miaka 20, Ali Ferej Tamim.   
    “Tumeshatoa maagizo kwa ZFA wilaya zote kuwa zianze maandalizi ya chaguzi hizo ili  itakapofika Disemba 27, ziwe zimemaliza kazi hiyo na kubakia uchaguzi ngazi ya taifa,” alisema Ravia.
    Alivitaka vyama na kamati hizo kutumia vyema muda uliopangwa wakati ZFA Taifa ikiendelea na mchakato wa kuzifanya chaguzi hizo katika siku moja ili kuweza kupatikana wajumbe wa mkutano mkuu kwa wakati.
    Alisema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, wajumbe wa mkutano mkuu wa chaguzi za wilaya, ni klabu zinazoshiriki ligi za madaraja mbalimbali wilayani.
    Kwa upande wa ngazi ya taifa, alisema wajumbe ni Makatibu na Wenyeviti wa wilaya, wajumbe watakaochaguliwa kuwakilisha wilaya zao katika ZFA, wawakilishi wa kamati za kudumu na mjumbe kutoka umoja wa klabu za soka.
    Akizungumzia mchakato wa marekebisho ya katiba ya chama hicho, Ravia alisema unaendelea vyema na kwamba kazi ya kuandaa rasimu imeshamalizika na tayari imetumwa kwa wadau wake, na kwamba baadhi yao wameshaanza kuipitia na kuitolea maoni.
    Alieleza kuwa, chama kinaendelea kuwasiliana na Baraza la Taifa la Michezo  Zanzibar (BTMZ) ili kuweza kukamilisha mchakato huo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UCHAGUZI MKUU ZFA JANUARI 3 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top