• HABARI MPYA

    Friday, September 26, 2014

    AZAM TV IMEFUNGUA MIANYA YA NEEMA LIGI KUU, LAKINI…

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    HISTORIA ya udhamini katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaanzia mwaka 1996, ilipojitokeza kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Safari Lager. 
    Ligi Kuu ikawa inaitwa Safari Lager Premier League, hata hivyo TBL iliamua kuachana na michuano hiyo mwaka 2001, baada ya aliyekuwa Waziri anayehusika na michezo wakati huo, Profesa Juma Kapuya kuvunja kanuni kwa kuongeza timu za kushiriki hatua ya pili ya michuano hiyo, kutoka timu sita hadi nane.
    Mwaka uliofuata, Ligi Kuu ikaangukia mikononi mwa kampuni ya simu ambayo ndiyo ilikuwa inaingia nchini wakati huo, Vodacom na udhamini wao umedumu tangu wakati huo, tena ukiboreshwa siku hadi siku.

    Mkurugenzi wa Azam Media Limited, Abubakar Bakhresa kulia akipeana mikono na aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage (kushoto) wakati wa kusaini Mkataba wa kipindi cha Simba TV mwaka jana. Katikati ni Mwanasheria wa Azam, Shani Chrstoms.

    Bado fungu la Vodacom halikutosha kuondosha matatizo katika Ligi yetu, kulikuwa kuna malalamiko ya fedha zinazotolewa ni chache na wakati mwingine zinachelewa pia.
    Ikawa rahisi Ligi yetu kutawaliwa na timu mbili kubwa- Simba na Yanga kwa sababu zenyewe wakati wowote, popote zinapocheza huvuna mapato mengi ya milangoni.
    Timu ambazo ziko dhaifu kiuchumi hazikuweza hata kuunda timu nzuri, achilia mbali kuziandaa vizuri- hivyo ikawa ni ligi ya piga ua, ama bingwa Simba au Yanga SC.
    Mtibwa Sugar ilikuwa timu ya kwanza kuchukua ubingwa wa Bara nje ya Simba na Yanga kwa mara ya kwanza mwaka 1999 tangu Coastal Union ya Tanga ilipofanya hivyo mwaka 1988.
    Na Mtibwa ina rekodi ya kipekee- kwamba ni timu pekee nje ya Simba na Yanga kutwaa mfululizo taji la Ligi Kuu, Waingereza wanaita ‘back to back’ jambo ambalo limewashinda hata Manchester City hadi sasa licha ya uwekezaji mkubwa.
    Azam FC ikawa timu ya kwanza kutwaa ubingwa wa Bara nje ya Simba na Yanga msimu uliopita, tangu Mtibwa Sugar mwaka 2000.
    Hii ni picha halisi kwamba udhaifu wa Ligi Kuu unatoa mwanya kwa Simba na Yanga kutawala, kwa sababu tu ni timu zenye mashabiki na zinavuna fedha za viingilio- inakuwa rahisi kujipanga kucheza Ligi Kuu.
    Wazi Ligi Kuu inahitaji fedha zaidi ili kujikuza na kuifanya yenye ushindani zaidi- shukrani kwao Azam Media Limited walioibuka msimu uliopita kuongeza fedha katika Ligi Kuu kwa kununua haki za matangazo ya Televisheni.
    Kila klabu ya Ligi Kuu inapata Sh. Milioni 100 na ushei kutoka Azam Media wanaorusha Ligi Kuu kupitia Azam TV- kwa ligi yetu ya miezi sita, wazi hili ni fungu zuri.
    Awali, Ligi Kuu haikuwahi kuuza haki za matangazo ya televisheni- wakati fulani Super Sport walikuwa wanaibuka kuonyesha bure mechi za ligi hiyo, kwa ‘gia’ eti wanaitangaza na kuwatangaza wachezaji waonekane, wapate soko.
    TV za nyumbani zilipewa nafasi ya kununua haki za matangazo ya Ligi Kuu wakati fulani na Star TV waliwahi kushinda tenda, lakini dau walilolipa kwa ligi nzima wakati huo haliingii kwa dau ambalo Azam FC wanatoa kwa timu moja tu kwa msimu.
    Hapa inajiainisha yenyewe namna ambavyo Azam TV imekuja kuipiga jeki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, maarufu VPL.
    Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited, Rhys Torrington kushoto akimkabidhi hundi ya malipo ya klabu, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Silas Mwakibinga kwa ajili ya haki za matangazo ya Televisheni ya msimu huu

    Faida ya ziada, kwa Azam Media Limited kununua haki za matangazo ya Ligi Kuu- inakwenda kumlinda mdhamini, Vodacom ambaye wakati fulani ziliibuka tetesi atajitoa aendelee kujitangaza kupitia mashindano hayo. 
    Lakini pia, kama Idara ya Masoko ya TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na Bodi ya Ligi pia- watakuwa na watu ‘shapu’ wanaweza kupata dili nyingine pia za kumwaga fedha katika ligi hiyo, kwa sababu sasa kuna Televisheni inayorusha matangazo ya ligi.
    Tuna kila sababu ya kusema asante Azam Media Limited kwa niaba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, lakini je, Bodi ya Ligi na TFF wanatumiaje mwanya huo kupata wadhamini zaidi wa michuano hiyo mikubwa nchini? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM TV IMEFUNGUA MIANYA YA NEEMA LIGI KUU, LAKINI… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top