• HABARI MPYA

    Saturday, September 27, 2014

    KIVUMBI LIGI KUU CHAENDELEA LEO; SIMBA SC WANA KAZI MBELE YA POLISI YA DANNY MRWANDA, AZAM FC NA RUVU SHOOTING, YANGA WAO KESHO TAIFA NA PRISONS TISHIO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara unatarajiwa kuendelea leo kwa nyasi za viwanja vitano kuwaka moto.
    Mabingwa watetezi, Azam FC watakuwa kwenye Uwanja wa nyumbani, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuwakaribisha Ruvu Shooting ya Pwani.
    Ruvu waliianza Ligi Kuu kwa kipigo cha nyumbani cha mabao 2-0 kutoka kwa Prisons ya Mbeya, wakati Azam FC walianza na ushindi wa 3-1 dhidi ya Polisi Morogoro iliyorejea Ligi Kuu msimu huu.
    Ikumbukwe, msimu uliopita Azam FC ilitangazia ubingwa kwenye Uwanja wa Ruvu, Mabatini, Mlandizi mkoa wa Pwani na hapana shaka kocha Mkenya, Thom Olaba atataka kulipa kisasi Chamazi leo.
    Kocha Mcameroon wa Azam FC, Joseph Marius Omog ataendelea kuwakosa Nahodha wake, John Bocco ‘Adebayor’ na Mhaiti, Leonel Saint Preux ambao ni majeruhi.
    Simba SC itawakosa Ivo Mapunda, Emmanuel Okwi na Paul Kiongera leo

    SIMBA SC VA POLISI MORO TAIFA
    Baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa ufunguzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba SC itajaribu kusahihisha makosa yake mbele ya Polisi Morogoro leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Bahati mbaya kwao Wekundu wa Msimbazi ni kwamba, hata Polisi Moro itaingia Uwanja wa Taifa na hasira za kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Azam FC katika mchezo wa kwanza.
    Mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Danny Mrwanda ambaye mwaka juzi alisajiliwa tena akatemwa kabla ya Ligi kuanza na kuamua kutimkia Vietnam, bila shaka leo atataka kulipa kisasi.
    Mrwanda ambaye alionyesha uwezo dhidi ya Azam FC, wazi leo atakuwa mwiba mbele ya mabeki wa Simba SC- akishirikiana na wakali wengine kama Bantu Admin na Suleiman Kassim ‘Selembe’.
    Safu ya ulinzi ya timu ya kocha Mohamed ‘Adolph’ Rishard, inatarajiwa kuendelea kuongozwa na beki mkongwe Lulanga Mapunda, ambaye pia ni Nahodha wa timu.
    Kocha Mzambia, Patrick Phiri atawakosa wachezaji wanne wote muhimu, kipa Ivo Mapunda, beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, kiungo Haroun Chanongo na mshambuliaji Paul Kiongera ambao ni majeruhi.
    Wakati huo huo, mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi hadi jana alikuwa hajapatiwa kibali cha kufanya kazi katika klabu hiyo- maana yake naye yuko shakani kucheza leo.
    Lakini bado usajili mzuri uliofanywa na Simba SC unawafanya wabakie na kikosi imara chenye uwezo wa kuvuna pointi mbele ya Polisi bila hata ya watano hao.
    Pengo la Ivo litazibwa na kipa bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Hussein Sharrif ‘Cassilas’, nafasi ya Issa ataendelea kucheza Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, wakati Twaha Ibrahim anaweza kucheza badala ya Chanongo na Elias Maguri akaziba pengo la Kiongera.

    MTIBWA SUGAR NA NDANDA FC
    Baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga SC Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Mtibwa Sugar leo itakuwa kwenye Uwanja wake halisi wa nyumbani, Manungu, Turiani kuikaribisha timu mpya katika Ligi Kuu, Ndanda FC ya Mtwara.
    Ndanda imeonyesha ni timu hatari baada ya kuanza Ligi Kuu kwa ushindi wa 4-1 ugenini, dhidi ya Stand United Uwanja wa Kambarage, Shinyanga. 
    Timu hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Bin Slum Tyres Limited, mashabiki wengi wa soka nchini leo watataka kujua matokeo yake, ili kuthibitisha kama ni wakali kweli, au waliwaotea Stand. 

    MBEYA CITY NA COASTAL UNION SOKOINE:
    Baada ya wote kuanza na sare katika mechi za kwanza, Mbeya City wakitoka 0-0 na JKT Ruvu nyumbani na Coastal Union wakitoka 2-2 na Simba SC Dar es Salaam, leo kila timu itasaka ushindi wa kwanza katika msimu huu wa Ligi Kuu.
    Mbeya City ya kocha Juma Mwambusi ambayo ilikuwa tishio msimu uliopita ikicheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza tangu ipande, leo itahitaji kurejesha imani ya mashabiki wake kwa kushinda.
    Lakini Coastal nao, chini ya makocha watatu Wakenya, Yussuf Chipo, Ben Mwalala na Razack Ssiwa, watahitaji kuonyesha kwamba msimu huu wamepania kurudia ya mwaka 1988, walipotwaa ubingwa wa ligi hiyo.  

    MGAMBO JKT NA STAND UNITED MKWAKWANI
    Mgambo JKT iliyonusurika kushuka daraja msimu uliopita, msimu huu imeonekana kujiimarisha baada ya kuanza na ushindi dhidi ya timu ngumu, Kagera Sugar na leo itacheza kwa mara ya pili mfululizo nyumbani dhidi ya timu kutoka Kanda ya Ziwa Victoria.
    Mgambo wataikaribisha Stand United ya Shinyanga iliyoanza na kipigo cha mabao 4-1 nyumbani kutoka kwa Ndanda FC waliyopanda nayo Ligi Kuu pamoja na Polisi Moro. 
    Yanga SC watajiuliza kwa Prisons kesho

    YANGA KUJIULIZA JUMAPILI; Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea Jumapili kwa mechi mbili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga SC wakiikaribisha Prisons ya Mbeya na Chamazi, JKT Ruvu wakiikaribisha Kagera Sugar.
    Yanga SC ilianza na kipigo cha ugenini kutoka kwa Mtibwa Sugar mabao 2-0, wakati Prisons ilishinda ugenini Mlandizi mkoani Pwani 2-0 pia dhidi ya wenyeji Ruvu Shooting.
    Kiungo Mbrazil Andrey Coutinho na mshambuliaji mzalendo, Jerry Tegete wanatarajiwa kurejea uwanjani leo, baada ya kukosa mechi mbili zilizopita kwa sababu ya maumivu.
    Wawili hao, walikuwa nje wakati Yanga SC ikitwaa Ngao ya Jamii Septemba 14, mwaka huu kwa kuichapa Azam FC 3-0 na katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu, timu yao ikilala 2-0 mbele ya Mtibwa Sugar Morogoro.   
    Lakini wakati wawili hao wakirejea, beki Oscar Joshua na mshambuliaji Hussein Javu nao kesho watachukua nafasi za Coutinho na Tegete jukwaani kwa sababu ni majeruhi.
    Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, JKT Ruvu iliyoanza kwa sare ya 0-0 na Mbeya City, itaikaribisha Kagera Sugar iliyoanza kwa kipigo cha Mgambo Tanga.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIVUMBI LIGI KUU CHAENDELEA LEO; SIMBA SC WANA KAZI MBELE YA POLISI YA DANNY MRWANDA, AZAM FC NA RUVU SHOOTING, YANGA WAO KESHO TAIFA NA PRISONS TISHIO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top