• HABARI MPYA

    Tuesday, September 30, 2014

    OSCAR JOSHUA NA JAVU WAANZA MDOGO MDOGO YANGA SC, DAKTARI AWAPA SIKU NNE KABLA YA KUWAKABIDHI KWA MAXIMO

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    BEKI wa kushoto wa Yanga SC, Oscar Joshua na mshambuliaji wa timu hiyo, Hussein Javu wameanza mazoezi mepesi baada ya kupata nafuu maumivu yao.
    Wawili hao walikuwa nje wakati Yanga SC ikipata ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumapili wa mabao 2-1 dhidi ya Prisons ya Mbeya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Hiyo ilifuatia Oscar kuumia katika mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar Yanga SC ikilala 2-0 Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Javu kuumia mazoezini baada ya mchezo huo.
    Daktari wa Yanga SC, Sufiani Juma ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, wachezaji hao wameanza mazoezi mepesi leo baada ya kupata nafuu.
    Oscar Joshua ameanza mazoezi mepesi Yanga SC

    Sufiani amesema wawili hao wataendelea na programu hiyo kwa siku nne na baada ya hapo, Kocha Mkuu, Mbrazil Marcio Maximo ataamua mustakabali wao.
    Yanga SC inatarajiwa kushuka tena dimbani Jumapili, kumenyana na JKT Ruvu ya Pwani katika mfululizo wa Ligi Kuu.
    Ikiwa na pointi tatu ilizovuna katika mechi mbili, Yanga SC itakutana na JKT yenye pointi moja iliyovuna katika sare ya 0-0 na Mbeya City Uwanja wa Sokoine, Mbeya kabla ya kufungwa 2-0 na Kagera Sugar Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam Jumamosi.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OSCAR JOSHUA NA JAVU WAANZA MDOGO MDOGO YANGA SC, DAKTARI AWAPA SIKU NNE KABLA YA KUWAKABIDHI KWA MAXIMO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top