• HABARI MPYA

    Saturday, September 20, 2014

    AZAM YAANZA VYEMA LIGI KUU BARA, POLISI WACHAPWA 3-1 CHAMAZI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara leo wameanza vyema mbio za kubakiza taji lao, baada ya kuichapa Polisi Morogoro mabao 3-1 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Ushindi huo unaomfuta machozi kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog baada ya kufungwa 3-0 na Yanga SC katika mchezo wa Ngao ya Jamii ulitokana na mabao ya Didier Kvumbangu mawili na Aggrey Morris.
    Azam walikwenda kupumzika wakiwa wanaongoza mabao 2-0, Kavumbangu akianza kufunga dakika ya 14 akiunganisha pasi ya Kipre Tchetche katikati ya beki na kipa wa Polisi.
    Shujaa; Didier Kavumbangu akishangilia baada ya kuifungia Azam FC mabao mawili katika ushindi wa 3-1
    Didier Kavumbangu akimtoka beki wa Polisi leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi
    Beki Aggrey Morris akaipatia bao la pili Azam FC dakika ya 23 aliyemalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Kipre Tchetche kufuatia beki Gardiel Michael kuchezewa rafu na Bantu Admin.
    Baada ya mabao hayo mawili ya haraka haraka, kocha wa Polisi Morogoro, Mohammed Adolph ‘Rishard’ alimpumzisha kiungo Bantu Admin na kumuingiza James Mganda.
    Mabadiliko hayo kidogo yaliituliza Polisi na kuanza kufika kwenye lango la Azam, ingawa hawakufanikiwa kupata bao hadi dakika 45 za kwanza zilipokamilika. 
    Mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Danny Mrwanda alidhibitiwa vikali na mabeki wa Azam leo.   
    Kipindi cha pili, Azam FC ilirudi vizuri na kusukuma mashambulizi mfululizo langoni mwa Polisi, lakini mshambuliaji Kipre Tchetche alikosa mabao matatu ya wazi.
    Nahoda Bakari aliipatia bao Polisi dakika ya 60 baada ya kuanzishiwa kona fupi na kumtungua kwa shuti la umbali 22 kipa Aishi Manula.
    Didier Kavumbangu aliifungia bao la tatu Azam FC dakika ya 90 akimalizia krosi ya Farid Malik.
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, David Mwantika, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao/Khamis Mcha ‘Vialli’ dk72, Mudathir Yahya, Didier Kavumbangu, Kipre Tchetche/Farid Malik dk72 na Salum Abubakar.
    Polisi Moro; Tony Kavishe, Rogeri Fred, Simon Fanuel, Ally Feruzi Telu, Lulanga Mapunda, Said Jella, Bantu Admin/James Mganda dk22, Nahoda Bakari/Suleiman Kassim ‘Selembe’ dk65, Danny Mrwanda, Machaku Salum na Nicholas Kabipe/Edgar Charles dk65.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM YAANZA VYEMA LIGI KUU BARA, POLISI WACHAPWA 3-1 CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top