• HABARI MPYA

    Thursday, December 06, 2012

    WASIWASI WA UPANGAJI MATOKEO NUSU FAINALI CECAFA TUSKER CHALLENGE

    Kocha wa Uganda, Mscotland Bobby Williamson kichwa kinamuuma akifikiria Stars

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    WAKATI Nusu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge zinafanyika leo mjini hapa, umeibuka wasiwasi mkubwa wa upangwaji matokeo kwa lengo la kuzikutanisha Kenya na Uganda katika fainali.
    Kenya itaanza kumenyana na Zanzibar saa 10:00 jioni na baadaye Uganda itamenyana na Tanzania Bara saa 12:00 jioni kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, mjini hapa.
    Habari za kiuchunguzi ambazo zimefikia BIN ZUBEIRY, zimesema kwamba kwa sababu mashindano haya hayakuwa na mahudhurio mazuri ya watu, maana yake CECAFA na wenyeji FUFA wamepata hasara, wanataka kutafuta namna ya kupata fedha angalau kidogo kwenye mechi ya mwisho.
    Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye, kweli wamepanga matokeo?
    Na wanaamini bila kuwapo mwenyeji kwenye fainali, mechi haitakuwa na mvuto kabisa mjini hapa, hivyo inadaiwa kuna mpango maalum wa kuibeba Uganda iifunge Bara iingie fainali.
    Lakini pia inaelezwa kutokana na upinzani na ujirani wa Kenya na Uganda, wenyeji wanaamini fainali ikizikutanisha timu hizo itakuwa na mvuto- hivyo inadaiwa kuna maelekezo maalum kwa marefa waibebe Harambee Stars dhidi ya Zanzibar Heroes.
    Katibu wa CECAFA, Mkenya Nicholas Musonye hajapatikana kuzungumzia shutuma hizo, lakini BIN ZUBEIRY inaendelea kumtafuta ili kupata kauli yake juu ya hilo. Musonye ameonyesha ukereketwa wa wazi katika mashindano haya pindi timu yake, Kenya inapocheza mjini hapa, kwani inapokuwa inaelemewa huwa mnyonge sana.    
    Tayari kocha wa Bara, Mdenmark Kim Poulsen ametoa tahadhari ya kuomba uchezeshwaji wa haki katika mchezo wa leo jioni.
    “Vijana wamejiandaa vizuri kabisa na wote wako katika hali nzuri ya kucheza ila tunachoomba ni uchezeshaji wa haki kutoka kwa refa, maana tunacheza na wenyeji ambao wana watazamaji wengi,” alisema.
    Poulsen alisema timu zote mbili ni nzuri na iwapo muamuzi atachezesha vizuri basi utakuwa ni mchuano mkali.
    Mechi zote zitaonyeshwa na Televisheni ya kulipia, SuperSport ya Afrika Kusini, ambapo watazamaji watapata fursa nzuri ya kujionea mbivu na mbichi juu ya uchezeshaji wa marefa.  Mungu ibariki Tanzania. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: WASIWASI WA UPANGAJI MATOKEO NUSU FAINALI CECAFA TUSKER CHALLENGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top