• HABARI MPYA

  Ijumaa, Desemba 21, 2012

  KIUNGO AZAM NJE WIKI MBILI

  Waziri akisaidiwa na makipa wa timu yake kutoka uwanjani baada ya mechi juzi. Kulia Jackson Wandwi na kushoto Mwadini Ally

  Na Mahmoud Zubeiry, Kinshasa
  KIUNGO Waziri Salum wa Azam FC, atakuwa nje ya Uwanja kwa wiki mbili kufuatia kuumia katika mchezo wa juzi dhidi ya Real de Kinshasa kwenye Uwanja wa Martyrs mjini hapa.
  Daktari wa Azam FC, Mjerumani Paulo Gomez ameiambia BIN ZUBEIRY jana mjini hapa kwamba Waziri ameumia mfupa wa pembeni wa paja la kushoto na kwa sababu hiyo atakuwa nje kwa muda wiki mbili akipata matibabu.
  Kocha Muingereza Stewart Hall amepokea kwa masikitiko taarifa hizo, akisema Waziri ni mchezaji ambaye anainukia vizuri Azam na kumkosa katika mashindano haya litakuwa pigo kwake.
  Hata hivyo, Stewart alisema atatumia wachezaji wengine wakati akimsubiri kiungo huyo Mzanzibari apate ahueni.
  Waziri amecheza mechi zote tatu za Azam katika mashindano haya hadi juzi alipoumia dakika ya 43 na kutoka nje.
  Kiungo huyo amekuwa akionyesha soka maridadi katika mashindano haya na kuashiria kwamba ataibeba Azam katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho mwakani.
  Wachezaji wengine majeruhi Azam ni kiungo Mzanzibari pia, Abdulhalim Humud anayesumbuliwa na maumivu ya nyama za paja na mshambuliaji John Bocco, ambao wamebaki Dar es Salaam. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KIUNGO AZAM NJE WIKI MBILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top