• HABARI MPYA

  Jumamosi, Desemba 22, 2012

  STEWART AIACHA AZAM KINSHASA, AENDA KULA SIKUKUU NYUMBANI

  Stewart wa kwanza kushoto akifutiwa na Kali, Kocha wa Makipa Iddi Abubakar na Daktari, Paulo Gomez raia wa Ujerumani

  Na Mahmoud Zubeiry, Kinshasa
  KOCHA Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall ameondoka jana usiku mjini hapa kwenda kwao Uingereza kwa ajili ya sikukuu za Krisimasi na mwaka mpya, akiiacha timu inakabiliwa na mchezo wa fainali ya Kombe la Hisani hapa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY kabla ya kuondoka mjini hapa, Stewart alisema kwamba anamuachia timu hiyo msaidizi wake, Kali Ongala na anaamini atafanya kazi nzuri.
  Stewart alisema Kali ni mtu ambaye siku zote amekuwa akimuandaa kuwa kocha wa baadaye wa Azam na hii si mara ya kwanza kumuachia timu, kwani aliwahi kufanya hivyo mara kadhaa ikiwemo kwenye Kombe la Urafiki, ambalo aliiongoza timu kufika Fainali.
  “Siku moja nitaondoka Azam na kumuacha Kali awe kocha Mkuu, siku zote namtayarisha, namjengea kujiamini, naamini atakuwa kocha bora sana wa Azam, sina wasiwasi naye, namuachia timu na anaweza kurudisha Kombe Dar es Salaam,”alisema Stewart ambaye atarejea mwakani.
  Azam kesho itacheza fainali, baada ya jana kufanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti 5-4 Shark FC ya hapa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs.
  Nahodha Jabir Aziz Stima ndiye aliyekwenda kupiga penalti ya mwisho, Shark wakitoka kupoteza, kufuatia mpira kugonga mwamba. Aiziz aliwainua vitini wachezaji wenzake na makocha wake pamoja na viongozi wa wachache wa timu hiyo waliopo hapa kwa kupiga penalti maridadi iliyotinga nyavuni.
  Azam iliuanza mchezo huo vizuri na ikicheza kwa maelewano makubwa sambamba na kushambulia kwa kasi kutokea pembeni, kulia Kipre Herman Tchetche na kushoto Seif Abdallah.
  Hata hivyo, shambulizi la kushitukiza la Shark liliwapa bao la kuongoza dakika ya 16, lililofungwa na Ngulubi Kilua, baada ya mabeki wa Azam kudhani ameotea.
  Iliwachukua dakika 10 tu Azam kusawazisha bao hilo, mfungaji akiwa Gaudence Exavery Mwaikimba aliyeunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya nyota wa mchezo huo, Kipere Herman Tcheche kutoka wingi ya kulia.
  Baada ya bao hilo, Azam iliendelea kuwashambulia Shark na dakika ya 37, Kipre Tchetche aliifungia timu hiyo bao la pili, kufuatia kazi nzuri ya Mwaikimba. Mwaikimba alipokea mpira mrefu, akatuliza na kumtangulizia kwa mbele mfungaji, ambaye hakufanya makosa, alimchambua kipa wa timu inayomilikiwa na mdogo wa rais wa DRC, Joseph Kabila.       
  Hadi mapumziko, Azam ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-1 na kipindi cha pili Shark waliingia kwa kasi na kufanikiwa kusawazisha kwa penalti dakika ya 47, iliyotiwa nyavuni na Bukasa Kalambai, ambaye yeye mwenyewe alijiangusha kwenye eneo la hatari baada ya kuzongwa na beki David Mwantika.
  Baada ya dakika 90 kutimu timu hizo zikiwa zimefungana 2-2, sheria ya matuta ilichukua mkondo wake na wachezaji wote watano wa Azam waliopewa dhamana hiyo na kocha Muingereza Stewart Hall, walitimiza wajibu wao vizuri.
  Kipre Tchetche alifunga ya kwanza, Mwaikimba ya pili, Jaockins Atudo ya tatu, Himid Mao ya nne na Stima akapiga ya ushindi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: STEWART AIACHA AZAM KINSHASA, AENDA KULA SIKUKUU NYUMBANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top