• HABARI MPYA

  Jumapili, Desemba 23, 2012

  AZAM BINGWA KOMBE LA UHAI, NI FURAHA DABO DABO CHAMAZI


   Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali mstaafu Idd Kipingu akimkabidhi nahodha wa timu ya Azam FC, Abdul Mgaya kombe la Ubingwa wa  michuano ya Uhai Cup 2012 baada ya timu hiyo kuifunga Coastal Union ya Tanga kwa penalti 3-1 katika mchezo wa fainali ya vijana chini ya miaka 20 uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Katikati ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodgar Tenga. (Picha zote na Habari Msetoto Blog)

   Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah akimkabidhi zawadi ya mfungaji bora wa mashindano ya vijana chini ya miaka 20 ya Uhai Cup, Ramadhani Mkipalamoto wakati wa fainali ya michuano hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.
   Wachezaji wa Azam FC wakishangilia baada ya kukabidhiwa kombe lao.
   Golikipa wa Azam FC, Aishi Salum akiokoa moja ya hatari zilizoelekezwa langoni mwake.
  Mshambuliaji wa Coastal Union, Twaha Shekue akitafuta mbinu za kumtoka beki wa Azam FC, Samwel Mkomola

  Na Prince Akbar
  TIMU ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Azam, maarufu kama Azam Academy, imehitimisha wiki ya furaha kwa klabu hiyo, baada ya kunyakua ubingwa wa Kombe la Uhai, linaloshirikisha timu za vijana za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
  Azam Akademy imetwaa ubingwa huo, baada ya kushinda kwa penalti 3-1, kufuatia sare ya 2-2 na Coastal Union ya Tanga ndani ya dakika 120 za pambano kali na la kusisimua.
  Ushindi wa Azam Academy, unakuja siku moja tu baada ya kaka zao, Azam FC kutwaa ubingwa wa Kombe la Hisani jana mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa kuwafunga wenyeji Dragons FC kwa penalti 4-2, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.
  Jana Azam walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 12 kabla ya Dragons kusawazisha dakika ya 75 na katika mikwaju ya penalti, kipa Mwadini Ally alicheza mikwaju miwili ya Dragons, wakati Gaudence Mwaikimba, Himid Mao, Joackins Atudo na Samih Hajji Nuhu walifunga penalti za Azam.
  Katika mchezo wa leo, Azam ilimenyana kiume na Coastal ambayo inaonekana kuinukia vizuri katika uwekezaji kwenye soka ya vijana kabla ya bingwa kupatikana kwa mikwaju ya penalti.  
  Mapema asubuhi katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu, Simba waliokuwa mabingwa watetezi, waliifunga 3-0 Mtibwa Sugar na kunyakua nafasi hiyo.
  Aidha, Bakari Shime wa Coastal Union ametwaa tuzo ya Kocha bora, Mansur A. Mansur wa Coastal Union kipa bora, Ramadhan wa Simba aliyefunga mabao sita, ameibuka mfungaji bora, Ruvu Shooting timu yenye Nidhamu, Joseph Kimwaga wa Azam mchezaji bora na Isiaka Mwalile refa bora.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: AZAM BINGWA KOMBE LA UHAI, NI FURAHA DABO DABO CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top