• HABARI MPYA

  Ijumaa, Desemba 21, 2012

  AZAM KUTINGA FAINALI LEO DRC?

  Mwaikimba ataendelea kucheka na nyavu leo?

  Na Mahmoud Zubeiry, Kinshasa
  AZAM FC inashuka dimbani leo kumenyana na Shark FC katika Nusu Fainali ya Kombe la Hisani mjini hapa, kwenye Uwanja wa Martyrs.
  Awali, Shirikisho la Soka Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC), liliitaka Azam FC kucheza mechi moja zaidi, baada ya kufuzu Nusu Fainali, lakini baada ya majadiliano, mpango huo umefutwa na leo Wana Lamba Lamba wanacheza Nusu Fainali moja kwa moja.
  Azam iliingia Nusu Fainali juzi baada ya kuilaza Real de Kinshasa kwenye Uwanja huo huo wa Martyrs, shukrani kwao, washambuliaji Gaudence Mwaikimba na Seif Abdallah waliofunga mabao hayo, moja kila kipindi.
  Ikiongezewa nguvu na nyota wake watatu, Kipre Tchetche, Kipre Balou raia wa Ivory Coast na Mkenya, Joackins Atudo waliochelewa mechi mbili za awali, Azam juzi ilitawala mchezo na kama si rafu za wapinzani wao, ingevuna ushindi mtamu.
  Hadi mapumziko, tayari Azam walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na Mwaikimba dakika ya 21, ambaye aliunganisha pasi nzuri ya Kipre kutoka wingi ya kushoto.
  Hilo lilikuwa bao la pili kwa Mwaikimba, mshambuliaji wa zamani wa Kahama United, Ashanti United, Yanga, Prisons na Kagera Sugar katika mechi tatu za mashindano haya alizocheza, awali alifunga katika sare ya 1-1 na Dragons.
  Kipre Tchetche alilazimika kutoka nje ya Uwanja dakika ya 43 kutokana na rafu za wachezaji wa Real, nafasi yake ikichukuliwa na Samih Hajji Nuhu.
  Real walikuwa wakipiga kiatu haswa na kiungo Waziri Salum aliungana na Kipre Tchetche kuuacha Uwanja kabla ya filimbi ya kuugawa mchezo, ingawa nafasi yake ilichukuliwa na Uhuru Suleiman dakika ya kwanza ya kipindi cha pili.
  Awali ya hapo, refa Madila Achille alimtoa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 43 beki Muipalayi Igongo kwa kumchezea rafu mbaya Gaudence Mwaikimba, ambayo chupuchupu naye imtoe nje, kiasi cha kulazimika kumalizia mechi akichechemea.
  Kipindi cha pili, Azam waliendelea kuwafundisha soka Real na katika dakika ya 73, kazi nzuri ya Mwaikimba ilisaidia kupatikana bao la pili. Mpira mrefu uliopigwa na kipa Mwadini Ally, Mwaikimba aliumiliki vema, akatoa pasi pembeni kushoto kwa Hajji Nuhu ambaye aliingia ndani kidogo na kukata krosi maridadi iliyounganishwa kimiani na Seif.
  Humphrey Mieno alikuwa mwathirika mwingine wa rafu za Real, baada ya kulazimika kutoka nje dakika ya 77, akimpisha Abdi Kassim ‘Babbi’.
  Azam walionekana kuridhika baada ya kuwa wanaongoza mabao 2-0 na wakafanya uzembe uliowapa bao la kufutia machozi Real, lililofungwa na Bisole Panzu dakika ya 78.
  Katika mechi zake mbili za awali za Kundi B, Azam ilitoka 1-1 na Dragons na ikafungwa 2-0 na Shark FC.
  Nusu Fainali nyingine itachezwa kesho wakati Fainali na mechi ya kusaka mshindi wa tatu zitachezwa Jumapili na Azam itaondoka hapa Jumatatu kurejea nyumbani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: AZAM KUTINGA FAINALI LEO DRC? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top