• HABARI MPYA

  Alhamisi, Desemba 27, 2012

  YANGA YAPASWA KUMTAYARISHA KIPA WA AKIBA BAADA YA BERKO KUONDOKA

  Pongezi kwake kocha Mholanzi wa Yanga, Ernie Brandts kuwapa nafasi wachezaji chipukizi aliowapandisha kutoka kikosi cha pili, George Banda na Rehani Kibingu katika mchezo wa jana dhidi ya Tusker, akiendelea hivi atawainua mapema, kwani nao wanaonyesha wanaweza na wako tayari. Katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Bara, Yanga ilikuwa ina makipa wawili wa kuaminika, Yaw Berko raia wa Ghana aliyeuzwa FC St. Eloi Lupopo na Ally Mustafa ‘Barthez’ (PICHANI KULIA)ambaye amebaki kama kipa namba moja kwa sasa. Ukirejea nyuma kidogo katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Berko alidaka hadi Robo Fainali alipoumia na kumpisha Barthez ambaye alidaka hadi timu ikawa bingwa. Kwa sasa Berko hayupo, kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na hata Kombe la Kagame mwakani Kigali, Rwanda Yanga wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa tena na makipa wawili wa uhakika. Wengi walitarajia kipindi hiki kipa Said Mohamed (PICHANI KUSHOTO)angeanza kutayarishwa na hata katika mchezo wa jana dhidi ya Tusker alitarajiwa kudaka yeye, lakini ajabu akasimama Barthez langoni.
  Benchi la ufundi la Yanga, lijiulize kama halitaanza wakati huu kumtayarisha Said ambaye tayari Watanzania wanajua ni kipa mzuri, litafanya lini kazi hiyo? Mechi ya jana ilikuwa ni nzuri Said kudaka kwa sababu Tusker ni timu nzuri na mabingwa wa Kenya, lakini ajabu Barthez ameendelea kudaka hadi kwenye mechi mazoezi dhidi ya timu za mchangani kama Kijitonyama Stars.
  Au tuseme kipa huyo wa zamani wa Majimaji haaminiki mbele ya benchi la ufundi la klabu hiyo, na kama ni hivyo kipindi cha usajili cha dirisha dogo kimepita kwa nini hakuruhusiwa kuondoka na klabu ikasajili kipa mwingine?
  Siku Barthez akiumia ghafla uwanjani na mapema katika mchezo mgumu na muhimu, Yanga wasitarajie miujiza wakimuinua Said ghafla pia kwenda kuchukua nafasi. Wanatakiwa waanze kumuandaa taratibu.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: YANGA YAPASWA KUMTAYARISHA KIPA WA AKIBA BAADA YA BERKO KUONDOKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top