• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 26, 2012

  KABLA YA KUWAHUKUMU SAMATTA, ULIMWENGU...

  Na Mahmoud Bin Zubeiry

  HASIRA za mashabiki wa soka Tanzania zi wazi kwa sasa dhidi ya washambuliaji wawili chipukizi wa timu hiyo, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu ambao wote wanachezea Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Wachezaji hao hawakupatikana katika kikosi cha Bara kilichocheza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge Novemba hadi Desemba mwaka huu na hawakuwapo pia kwenye kikosi cha Muungano, Taifa Stars kilichocheza dhidi ya Zambia Jumamosi iliyopita.
  Kwa sasa, wawili hao wanachukuliwa kama hawana mapenzi kwa timu yao na mashabiki nchini wameanza kuonyesha hasira za wazi dhidi yao.
  Katika mchezo wa Taifa Stars na Zambia, wapo mashabiki walibeba mabango ya kuwakandia wachezaji hao, haswa Samatta.
  Siku zote, mtu anayechukiwa sana ni yule ambaye alipendwa awali- hivyo hata chuki dhidi ya Samatta zinatokana na kwamba Watanzania walimpenda sana, wakamuunga mkono na kumtakia kila la heri katika jitihada zake za kusaka mafanikio kisoka.
  Watanzania walitarajia makubwa kutoka kwake- kwamba angeisaidia mno timu ya taifa, angeitangaza nchi katika dunia ya soka kupitia mafanikio yake binafsi kutokana na kipaji chake.
  Lakini sasa hayo yameingia doa, kutokana na chuki hizo zilizoibuka dhidi yake na mwenzake na Ulimwengu, kwa kutofika katika kambi za taifa wanapoitwa.
  Siku zote mimi naamini, ni vema Watanzania tukawa na utamaduni wa kuyatazama mambo kwa kina, kuyajadili kwa mapana marefu, ili kuyapatia majibu sahihi katika lengo ya kuyatatua.
  Kwa sababu hiyo, sioni kama kuna mantiki yoyote kwa sasa kwetu kuanza kujenga chuki dhidi ya Samatta na Ulimwengu bila kupitia hatua hizo za msingi. Hawa vijana bado wadogo na kwa hakika taifa bado linawahitaji sana ni vema kuwa nao pamoja, kuliko kutaka kutengeneza mtafaruku.
  Sioni kama suala hilo limefikia huko tunapotaka kulifikisha, zaidi ya kutaka kuzipa nafasi hasira kufanya kazi kuliko hekima na busara.
  Nataka nikumbushe kitu kimoja, suala la hawa wachezaji kuja katika kambi za taifa linatokana na ruhusa ya klabu yao, Mazembe.
  Niliwahi kufanya mahojiano na Makamu wa Rais wa Mazembe, Mohamed Kamwanya kuhusu kuchelewa kwa Ulimwengu kuingizwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo, ambaye alisema kwamba mshambuliaji huyo alichelewa kwa sababu ya kiwango chake.
  Alisema kwamba, Ulimwengu kila anapopewa ruhusa ya kurejea Tanzania kujiunga na timu za taifa, kwanza huchelewa kurudi Lubumbashi na pia hurudi akiwa hayuko fiti.
  “Hicho ndio kinamchelewesha, lakini kama siyo hivyo angekuwa anacheza tu kama mwenzake. Na nyinyi watu wa vyombo vya habari mtusaidie, kwa sababu wachezaji wakija huko wanafanya anasa, wanarudi huku hawako fiti, sasa inakuwa mbaya,”alisema Kamwanya.
  Kabla ya hili sakata la juzi, awali Mazembe ilifikia hatua ya kuwazuia wachezaji wote hao, kurejea Tanzania kujiunga na timu za taifa, kwa sababu hata Samatta inaelezwa anaporejea nyumbani, akirudi Lubumbashi anakuwa ameshuka kiwango.
  Hali hiyo imetafsiriwa inatokana na wachezaji hao kufanya anasa wanapokuwa Dar es Salaam na chanzo ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchelewa kuwapa tiketi wachezaji hao, wanapomaliza majukumu yao ya kitaifa, hivyo wakati wanasubiri tiketi wanaishia kujirusha, kula bata kwa kwenda mbele.
  Kwa kuwa kipindi chote hicho wanakuwa hawafanyi mazoezi na wanaichosha miili yao kwa anasa, wanapoelekea Lubumbashi wanampa kazi kocha Lamine N’Diaye kuanza kuwatengeneza upya.
  Alipochoshwa na hali hiyo, N’Diaye aliweka ngumu, Uli hakurudi nyumbani kuichezea timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes na kwa kumkosa mpachika mabao wake huyo tegemeo, sisiti kusema ilichangia kwa kiasi kikubwa kutolewa na Nigeria katika mbio za kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika.
  Hilo liliwafanya TFF, walalamike sana hasa baada ya kumpiga ‘stop’ na Samatta pia kujiunga na kambi ya timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Botswana, ambao uliisha kwa sare ya 3-3 mjini Gabarone hadi kutishia kulifikisha suala hilo Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwani wamekiuka agizo la Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
  TFF walisahau kwamba, Mazembe ilikuwa ina hoja na lalamiko la msingi, ambalo naamini kesi hiyo ikienda popote, klabu hiyo bingwa Afrika mara nne, itashinda.
  Mchezaji ni mali ya klabu na kanuni zinatoa mwongozo mzuri juu ya ushiriki wao kwenye timu za taifa, hivyo hata vyama vya soka vina wajibu wa kuzitekeleza kanuni hizo.
  Bado wamekuwa hawajali hata umuhimu wa kuwarejesha mapema wachezaji wa nje baada ya kumaliza majukumu yao ya kitaifa.
  Natambua kuna mambo mawili hapa katika suala la wachezaji hawa, Samatta kusema anaumwa hawezi kujiunga na timu na pia kutorejea kujiunga na timu baada ya kuitwa. Nataka sote tutambue umuhimu wa wachezaji hawa kwanza, kabla ya kuanza kulijadili suala lao.
  Na baada ya hapo, ndipo twende kwenye hoja ya msingi bila ya jazba, tuanze na kutoonekana kwao kwenye Challenge na hili la juzi la Zambia.
  Samatta amesema anaumwa, sasa tunapokataa haumwi ina maana tunamchukulia yeye kama roboti au? Tunataka tu Samatta acheze hata katika mazingira hatarishi, mwisho wa siku tunasahau historia ya TFF na wachezaji wanapoumia, tangu inaitwa FAT.
  Wachezaji wangapi wamekwishatelekezwa baada ya kuumia na hata wa kizazi cha sasa kiasi cha wengine kama Stefano Mwasyika kufikia kuapa hatachezea tena timu hiyo?
  Lakini pia hatupaswi kusahau kwamba hawa vijana nao ni binadamu na mchezo wa soka umeundiwa mamlaka yake inayotambulika kisheria, hivyo kuna namna ya kuwasiliana nao yanapotokea matatizo kama haya.
  Binafsi sikuona umuhimu wa mchezaji yeyote anayecheza nje kuitwa katika kikosi cha Challenge au kilichomenyana na Zambia katika wakati huu ambao tunajiandaa na mechi za kufuzu za CHAN.
  Niliona ipo haja ya kuwa na kikosi ambacho tutakitumia kwenye mechi za kufuzu za CHAN, ambacho kitaundwa na wachezaji wa nyumbani pekee.
  Sijui Kim Poulsen amekuwa na woga kiasi gani hadi katika mechi kama hizi ambazo anapaswa kuandaa timu ya kumpigania kwenye mashindano mengine muhimu, anataka kuchanganya madawa.
  Lakini hiyo si hoja yangu leo, yalikuwa mapitio tu. Hoja yangu leo ni kuhusu Samatta na Ulimwengu, tusiwahukumu kabla ya kulitazama kwa jina suala lao na kulijadili kwa mapana marefu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KABLA YA KUWAHUKUMU SAMATTA, ULIMWENGU... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top