• HABARI MPYA

  Alhamisi, Desemba 20, 2012

  MWAIKIMBA ATAKA KUMSAIDIA USHINDI KIM POULSEN STARS

  Mwaikimba DRC

  Na Mahmoud Zubeiry, Kinshasa
  MSHAMBULIAJI mrefu, Gaudence Exavery Mwaikimba anayeng’ara kwenye michuano ya Kombe la Hisani hapa DRC, amesema kwamba bado ana uwezo mkubwa wa kuisaidia timu yake ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, lakini hawezi kuingilia maamuzi ya kocha Kim Poulsen.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY mjini hapa jana, Mwaikimba alisema kwamba uwezo wake siku zote upo juu kwa sababu ana kipaji na anajituma mazoezini, lakini hajui Kim anamfikiria vipi.
  “Tangu mimi nimeibuka katika soka ya nchi hii, hakuna kocha ambaye alikuja kufundisha timu ya taifa akaacha kuniita kwenye kikosi, nadhani hata huyu Kim bado hajaniona tu, lakini mwenzake Jan Borge Poulsen aliniita,”alisema.
  Mwaikimba alisema hawezi kulazimishwa kuitwa timu ya taifa kwa sababu ile ni timu ya Watanzania wote na Tanzania ina wachezaji wengi, ila roho itaendelea kumuuma kila timu itakapokuwa ikifanya vibaya wakati yeye ana uwezo wa kuisaidia.
  “Ni kweli Tanzania ina washambuliaji wengi, lakini mimi ni wa kipekee, kama ninakuwa kwenye timu na kocha akanitumia vizuri, lazima nitakuwa tishio. Sema tu tatizo makocha wengi wa hapa hawajiamini na wanashindwa kufanya kazi zao vizuri,”alisema.
  “Angalia Stewart (Hall, kocha wa Azam) huyu hapa, ndiye kanisajili hapa Azam na hadi kesho ananitumia na ananielekeza vizuri. Yaani mimi nauona umuhimu wangu kwake, inakuwa rahisi mtu kufanya kazi,”alisema.   
  Katika mechi tatu za mashindano ya Kombe la Hisani, Mwaikimba amefunga mabao mawili hadi sasa.
  Mwaikimba alikuwa mchezaji wa timu ya taifa kuanzia mwaka 2006 hadi 2010, ingawa wakati fulani mwaka 2009 aliwahi kutemwa na kocha Mbrazil, Marcio Maximo baada ya kiwango chake kushuka.
  Na kushuka kwa kiwango chake kulichangiwa na migogoro na kocha wa klabu yake ya zamani, Profesa Dusan Savo Kondic raia wa Serbia, kiasi cha kufikia kuhama timu.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MWAIKIMBA ATAKA KUMSAIDIA USHINDI KIM POULSEN STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top