• HABARI MPYA

    Sunday, December 23, 2012

    RAGE ANG'OKA TAREFA, KITUMBO BOSI MPYA WA SOKA TABORA

    Mwenyekiti aliyemaliza muda wake
    TAREFA, Alhaj Ismail Aden rage

    Na Prince Akbar
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeupongeza uongozi mpya wa Chama cha Soka Tabora (TAREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Desemba 22 mwaka huu).
    Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba, ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TAREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Tabora.
    Amesema TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TAREFA chini ya uenyekiti wa Yusuf Kitumbo aliyeshinda kwa kura 16 dhidi ya nane za Musa Ntimizi, na Paul Werema ambaye hakupata kura.
    “Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Tabora kwa kuzingatia katiba ya TAREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake,”.
    “Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF,”alisema Wambura.
    Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Yusuf Kitumbo (Mwenyekiti), Fate Remtulla (Katibu), Dick Mlimuka (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Razak Irumba (Mwakilishi wa Klabu TFF) na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao ni Eric Kabepele na Mwalimu Sizya.
    Wakati huo huo: Chama cha Soka ya Wanawake Tanzania (TWFA) kimetoa tuzo kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga na Meneja wa timu ya Taifa (Twiga Stars), Furaha Francis kutokana na mchango wao katika kuendeleza mchezo huo.
    Tuzo hizo zilitolewa katika Mkutano wa Uchaguzi wa TWFA uliofanyika Desemba 19 mwaka huu mjini Morogoro kutokana na mchango wao katika kuendeleza mpira wa miguu kwa wanawake nchini.
    “Ni dhahiri kazi ya kuendeleza soka ya wanawake ni wajibu wa Shirikisho (TFF), lakini Rais wa TFF alitoa kipaumbele zaidi na alijitoa kuhakikisha misingi imara ya kuendeleza soka ya wanawake inawekwa,” alisema Mwenyekiti wa TWFA, Lina Kessy.
    Pia Mkutano huo ulitambua na kumpa tuzo Furaha Francis ambaye amekuwa Meneja wa Twiga Stars kwa miaka minane mfululizo. Licha ya kuwa Meneja wa Twiga Stars, ametumia muda wake na kujitoa katika kuendeleza mpira wa miguu kwa wanawake.
    TWFA itaendelea kutumia michango yao katika mpira wa miguu kwa wanawake nchini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: RAGE ANG'OKA TAREFA, KITUMBO BOSI MPYA WA SOKA TABORA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top