• HABARI MPYA

  Jumapili, Desemba 30, 2012

  RIDHI AMEONA MBALI, YANGA BADO BURE TU!

  Na Bin Zubeiry

  MWENYEKITI wa Kamati ya Kusaidia timu za soka za vijana za taifa, Ridhiwani Kikwete, jana aliuzungumzia mfumo wa uendeshwaji wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam na kuweka bayana ni mbovu.
  Ridhi alisema wazi, mfumo haufai kwa sababu unategemea fedha za kuendesha klabu kutoka kwenye mfuko wa mtu mmoja.
  Akizungumza wakati anatoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) jana katika hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani Pwani, Kikwete alisema kwamba Yanga inahitaji kubadilika kutoka mfumo huo.
  Kikwete alisema ni afadhali mfumo wa uendeshwaji wa mahasimu wao wa jadi, Simba SC, ambao desturi yao ni kuchangishana.
  “Nilijaribu kufanya uchunguzi wa mfumo wa uendeshwaji wa klabu ya Yanga, nikashangazwa ni mfumo mbaya, kwa sababu unategemea mfuko wa mtu mmoja, afadhali Simba wao huwa wanachangishana,”alisema.
  Alichokisema Ridhiwani ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, NEC akiiwakilisha Wilaya ya Bagamoyo ni kitu ambacho kipo wazi, kwamba Yanga bado haina msingi imara.
  Na vema hili limezungumzwa na mtu mzito mapema, kabla ya uongozi mpya wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Alhaj Yussuf Manji haujamaliza hata mwaka mmoja, ili kama viongozi wao ni wasikivu, waitafutie misingi imara klabu.
  Lazima ifike wakati, Yanga iweze kujiendesha bila kutegemea mfuko wa mtu, na hapo ndipo itasaidia hata kuondoa ‘Miungu watu’ ndani ya klabu. Ndiyo, ndani ya Yanga kuna watu wanataka kuabudiwa kila siku, wakijua wao ndiyo wenye uwezo wa kuifanya timu isimame.
  Hili haliko sawa na kama alivyosema Ridhiwani, viongozi wapya wa Yanga wanatakiwa kuleta mapinduzi katika klabu.
  Yanga ni klabu ambayo inaweza kujiendesha kutokana na ukweli kwamba ni taasisi kubwa, ina rasilimali kuanzia ya watu na mali zisizohamishika.
  Jengo la Mafia, jengo la makao makuu ya klabu pale Jangwani pamoja na Uwanja wa Kaunda, vyote ni vitegauchumi vikubwa sana vinavyoweza kuifanya Yanga ijiendeshe.
  Ndiyo, Mwenyekiti wa Yanga, Manji alimtambulisha mkandarasi wa kujenga upya Uwanja wa Kaunda, lakini bado tunasubiri utekelezaji wake. Lakini pia, lazima iwekwe bayana, mkandarasi huyo anajenga Uwanja huo kwa makubaliano yapi na ni nani atakayegharamia fedha za ujenzi huo.
  Na je, anajitolea au anaikopesha klabu. Ndiyo, maana wana Yanga wasifurahie tu ahadi ya ujenzi wa Uwanja bila kujua kesho nini kitafuata. Wakati, fulani mwanachama mmoja wa Yanga, Abeid Falcons alitaka kuukarabati Uwanja wa Kaunda, lakini akazuiwa na uongozi chini ya Mwenyekiti wa wakati huo, Wakili Imani Madega, kwa sababu ilikuwa ni hatari kwa klabu.
  Kila siku nasema, Yanga si mali ya mtu. Ni mali ya watu, hivyo isitokee watu kwa sababu tu wamepewa dhamana ya kuongoza wakajisahau na kuichukulia kama ile ni mali yao. Hapana.
  Leo mambo bado yanakwenda holela tu Yanga na huwezi kuona dalili za mabadiliko kutokana na uongozi mpya. Wana Yanga bado wananunua jezi, kalenda na bidhaa nyingine kibao zenye nembo ya klabu, lakini haijulikani klabu inanufaika vipi.
  Iko wapi mikataba ya tenda hizi- zilitangazwa lini? Tuachane na hayo, Yanga inapata nini kutokana na mauzo ya bidhaa hizo?
  Miezi miwili iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alitoa taarifa ya mapato na matumuzi ya kipindi cha miezi mitatu cha kuwapo kwao madarakani, ikaonyesha Yanga inajiendesha kwa hasara- maana yake inategemea mfuko wa mtu.
  Lakini kwa nini klabu kubwa kama hiyo ijiendeshe kwa hasara? Bado siku chache baadaye, anaitisha Mkutano kutangaza kuingia mkataba na kampuni ya Prime Time Promotions isimamie mkutano Mkuu na kuiandalia klabu mechi za kirafiki za kimataifa kwa mkataba wa Sh Milioni 105.
  Huu ni mzaha, Yanga ina uwezo kuingiza Sh. Milioni 300 au zaidi katika mechi moja tu ya maana ya kirafiki itakayocheza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, iweje leo Prime Time ipewe tenda ya kuandaa mechi ambazo idadi yake haijulikani kwa Milioni 105 tu?
  Hizi ni dalili tosha za wanachama wa Yanga kuanza kupata shaka juu ya uongozi wao mpya, kama kweli utaweza kuivusha klabu katika hatua nyingine.
  Kama unashindwa kuongoza Yanga, yenye rasimimali kibao, kweli utaweza kuongoza timu kama Toto Africans?
  Yuko mtu anaitwa Rahim Kangezi ‘Zamunda’, huyu jamaa anavyoteseka na African Lyon unaona kabisa akiipata timu kama Yanga, ataifikisha mbali sana.
  Zamunda ana mipango na ni mtendaji, kitu ambacho viongozi wa Yanga wa sasa kama wanakosa hivi.  Lakini bado viongozi wa Yanga wanaweza kuwa karibu na Zamunda ili kujifunza kwa manufaa ya Yanga.  
  Ukienda kwenye masuala mengine ya kiutendaji Yanga, bado ni vurugu tupu. Makomandoo bado wanakumbatiwa, usajili mwingine unafanyika usio na tija kwa klabu, ili mradi tu kuna watu wamepewa dhamana, wao ndio wenye mamlaka na hakuna wa kuwaambia kitu.
  Ama kwa hakika Ridhiwani ameona mbali sana, mfumo wa uendeshaji Yanga ni mbovu. Tena kupita maelezo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: RIDHI AMEONA MBALI, YANGA BADO BURE TU! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top