Ngassa |
Na Mahmoud Zubeiry
YAMEISHA
salama, lakini! Simba SC na Azam FC zimefikia makubaliano ya kumuuza kwa pamoja
mshambuliaji Mrisho Ngassa kwenda El Merreikh ya Sudan, lakini ajabu mchezaji
huyo hapatikani kwenye simu ili kuhusishwa kwenye dili hilo.
Habari za
ndani ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka kwenye kikao cha pamoja kati ya
Simba na Azam leo, zimesema kwamba Merreikh imeongeza dau la kumnunua Ngassa
kutoka dola za Kimarekani 70,000 hadi 100,000, zaidi ya Sh. Milioni 150 za
Tanzania.
Baada ya
kuongeza dau hilo, Azam ilikutana na Simba kujadili pamoja ofa hiyo mpya na
kukubaliana kumuuza na kugawana nusu kwa nusu.
Upande wa
Azam uliwakilishwa na mmoja wa Wakurugenzi wa bodi ya klabu hiyo, wakati kwa
Simba waliwakilishwa na Makamu wao Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’.
Upande wa
maslahi ya mchezaji umeboreshwa pia, Ngassa sasa atapewa dola za Kimarekani Sh.
75, zaidi ya Sh. Milioni 110,000 kwa kusaini mkataba wa miaka miwili na mshahara
utabaki kuwa dola 4,000 (Sh. Milioni 6).
Habari zinasema
kwamba, baada ya makubaliano hayo, kesho Simba na Azam watasaini mkataba na Azam
na kumuuza rasmi mchezaji huyo.
Hata hivyo,
tangu wakati kikao hicho kinaendelea jioni ya leo, Ngassa alikuwa akitafutwa
ili kuhusishwa, lakini hakupatikana kwenye simu.
Wasiwasi umeibuka
kwamba huenda Ngassa anaweza akawa ameghairi mpango wa kwenda Merreikh kutokana
na ushauri mbaya wa watu wake karibu. Mchezaji mmoja wa timu ya taifa, aliiambia
BIN
ZUBEIRY leo kwamba Ngassa anafikiria kuachana na mpango wa kucheza
Sudan, kwa sababu anasikia ni nchi ya Kiislamu na haina starehe.
Wapembuzi wa
mambo wanasema kwamba, ilipofikia Ngassa anahitaji ushauri nasaha, kwani nafasi
aliyopata ni adimu na ni muhimu kwa taifa na hata kwa maslahi yake binafsi.
Achilia mbali
maslahi mazuri, lakini anakwenda kucheza timu ya ushindani ambayo itakuza kiwango
chake aweze kuisaidia timu ya taifa pia. Merreikh ni timu ambayo karibu kila mwaka
inashiriki Ligi ya Mabingwa.
Dili la
Ngassa kwenda Merreikh awali liliingia katika mgogoro, baada ya Azam kumuuza
bila kuishirikisha Simba.
Ikumbukwe, Azam
walimtoa kwa mkopo Ngassa mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu baada ya kukerwa na
kitendo cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, katika
Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi
ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alifanya
hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea benchi na kuiwezesha Azam
kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa na Yanga 2-0, naye kwa mara
nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga, hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.
Ilielezwa
kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa mkopo mchezaji huyo, ingawa
baadaye Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka mmoja aliobakiza mchezaji
huyo Azam FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa kumsainisha kwa Sh. Milioni
30, kati ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18 akipewa gari.