Cannavaro baada ya kukosa penalti jana |
Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
NAHODHA wa
Zanzibar, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema kwamba anamshukuru sana kipa wao,
Mwadini Ally kwa kucheza penalti ya Abdul Fiston wa Burundi jana, kwani
vinginevyo walikuwa wamekwishatolewa kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika
Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge.
“Mimi
nilipokosa tu penalti kwa kweli mwili ulikufa ganzi na kuamini sasa safari ya
kurudi Zanzibar imeiva na mimi ndiye nimewaangusha wenzangu. Sikuwa na raha tena,
lakini nguvu ziliniijia baada ya Mwadini kucheza penalti,”alisema Cannavaro
alipozungumza na BIN ZUBEIRY jana Uwanja wa Lugogo.
Nahodha huyo
wa Yanga SC ya Dar es Salaam, alisema kwamba baada ya kuitoa Burundi sasa
anaamini Kombe la Challenge litakwenda Zanzibar, kwani haoni timu nyingine ya
kuwasumbua wao katika mashindano haya.
Zanzibar
jana ilikata tiketi ya kutinga Nusu Fainali baada ya kuichapa Burundi kwa
penalti 6-5 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 na sasa itacheza
na mshindi kati ya Kenya na Malawi katika Nusu Fainali.
Shujaa wa
Zanzibar jana alikuwa ni Abdallah Othman aliyefunga penalti ya mwisho, baada ya
kipa Mwadini Ally kupangua penalti ya Abdul Fiston wa Burundi.
Manahodha wa
timu zote, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Zanzibar na Suleiman Ndikumana wa
Burundi walipoteza penalti zao jana.
Ndikumana
alikuwa wa kwanza kwenda kupiga na mkwaju wake ukaota mbawa na kupaa juu ya
lango, wakati wenzake waliofunga mbali na Fiston kupoteza ni Steve Nzigamasabo,
Amisi Tambwe, Chris Nduwarugira, Leopold Nkurinkiye na Gael Duhatindavyi.
Upande wa
Zanzibar Heroes, Khamis Mcha ‘Vialli’ alikwenda kufunga penalti ya kwanza ya
Zanzibar, Adeyom Saleh Mohamed akafunga ya pili, Jaku Juma akafunga ya tatu,
kabla ya Cannavaro kumpelekea mikononi mkwaju wake kipa Arthur Arakaza wa
Burundi, Samir Hajji Nuhu akafunga ya tano, Aggrey Morris akafunga ya sita na
Othman kutumbukiza nyavuni ya ushindi.