• HABARI MPYA

    Friday, June 28, 2019

    SIMBA SC YASAJILI MCHEZAJI MWINGINE KUTOKA KLABU YA LIGI DARAJA LA NNE BRAZIL

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imesajili mchezaji mwingine kutoka Brazil, ambaye ni beki Tairone Santos da Silva mwenye umri wa miaka 30 aliyesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na mabingwa hao wa Tanzania Bara.
    Tairone Santos da Silva anajiunga na Simba SC akitokea klabu ya Atletico Cearense FC inayocheza Ligi Daraja la Nne nchini Brazil, maarufu kama Serie D.
    “Kazi ya kuimarisha kikosi cha Mabingwa wa nchi inaendelea kama kawaida, beki Tairone Santos da Silva (30) amesaini mkataba wa miaka miwili kuchezea Msimbazi. @tairone89 amejiunga na klabu yetu akitokea ya Atlético Cearense FC ya nchini kwao Brazil,”imesema taarifa ya Simba SC leo.

    Tairone Santos da Silva anakuwa Mbrazil wa tatu kusajiliwa Simba SC baada ya beki Gerson Fraga Vieira kutoka klabu ya ATK ya Ligi Kuu ya India na mshambuliaji Wilker Henrique da Silva kutoka Bragantino ya Ligi Daraja la Nne pia nchini Brazil.
    Na kwa ujumla Silva anakuwa mchezaji mpya wa sita kusajiliwa Simba SC baada ya kipa Beno Kakolanya kutoka Yanga, beki Kennedy Wilson Juma kutoka Singida United za nyumbani, kiungo Msudan, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman na Vieira na Henrique da Silva.
    Pamoja na kusajili nyota wapya, Simba SC imewaongezea mikataba baadhi ya wachezaji wake wa msimu uliopita, wakiwemo kipa Aishi Manula, mabeki Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Nahodha Msaidizi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala, viungo Jonas Mkude, Mzambia Clatous Chama na washambuliaji Nahodha Mkuu, John Bocco na Meddie Kagere raia wa Rwanda.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YASAJILI MCHEZAJI MWINGINE KUTOKA KLABU YA LIGI DARAJA LA NNE BRAZIL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top