• HABARI MPYA

    Sunday, June 30, 2019

    SIASA NA ITIKADI ZAKE VISIRUHUSIWE SANA KUINGILIA KWENYE MICHEZO

    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars itaingia kwenye mchezo wa mwisho wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 dhidi ya Algeria kesho kukamilisha ratiba na kusaka heshima.
    Hiyo ni baada ya kuchapwa mabao 3-2 na Kenya katika mchezo wake wa pili wa Kundi C Alhamisi wiki hii Uwanja wa Juni 30 mjini Cairo.
    Baada ya kufungwa 2-0 na Senegal kwenye mchezo wa kwanza Juni 23, sasa Taifa Stars itaingia kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Algeria Julai 1 kukamilisha ratiba na kusaka heshima, wakati Kenya itahitaji ushindi mbele ya Senegal kuangalia uwezekano wa kusonga mbele kufuatia kupoteza mechi ya kwanza.

    Alhamisi ya Juni 27, kiungo mshambuliaji wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Simon Happygod Msuva alianza kuifungia Taifa Stars bao zuri na la mapema dakika ya sita tu ya mchezo.
    Lakini mshambuliaji wa Kashiwa Reysol ya Japan aliyewahi kuchezea Girona ya Hispania kwa mkopo, Michael Ogada Olunga aliisawazishia Harambee Stars kwa tik tak dakika ya 39 akitumia makosa ya kipa wa Simba SC, Aishi Salum Manula kutema mpira. 
    Hata hivyo, bao hilo la mshambuliaji huyo wa zamani wa Tusker, Thika United, Gor Mahia za nyumbani kwao, Kenya zote akicheza kwa mkopo kutroka kademi ya Liberty Sports kabla ya kuuzwa Djurgardens IF ya Sweden ambayo nayo ilimuuza Guizhou Zhicheng ya China halikudumu sana.
    Kwani dakika moja baadaye, Nahodha wa Tanzania na mshambuliaji wa KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Ally Samatta aliifungia bao la pili Taifa Stars baada ya jitihada binafasi akiwapangua mabeki wa Kenya na kumtungua kwa shuti kali kipa wa Saint George ya Ethiopia, Patrick Musotsi Matasi.
    Kipindi cha pili Harambee Stars walio chini ya kocha Mfaransa, Sebastien Migne walikuwa na moto na kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Taifa Stars inayofundishwa na Mnigeria, Emmanuel Amunike.
    Na jitihada zao zilizaa matunda dakika ya 62 baada ya kiungo wa Cercle Brugge ya Ubelgiji, Johanna Ochieng Omolo kufunga bao la kusawazisha akimalizia kazi nzuri ya mshambuliaji wa Beijing Renhe ya China, Ayub Timbe Masika aliyewahi kucheza Lierse SK ya Ubelgiji.
    Olunga akaifungia Harambee Stars bao la ushindi dakika ya 80 akimalizia kazi nzuri ya mtokea benchi, kiungo wa IF Brommapojkarna ya Sweden, Eric Johana Omondi.
    Matokeo hayo yaliwaumiza mno Watanzania – na kwa kuzingatia timu ilifungwa 2-0 na Senegal kwenye mchezo wa kwanza, hasira zao zikaishia kukandia benchi la ufundi na wachezaji.
    Watanzania wakasahau kwamba nchi yao ilikuwa inashiriki AFCON kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 39 na hawakuzingatia walikutana na timu zinazowazidi uwezo.
    Tunajishusha mno, tunaona hatuwezi kabisa tu kwa sababu ya kupoteza mechi zote mbili za kwanza za Kundi C, kiasi kwamba tunasahau tulipigana kwa miaka 39 kupata tena tiketi ya AFCON.
    Mwaka huu Uganda wanashiriki AFCON kwa mara ya pili mfululizo baada ya kurejea kwa mara ya kwanza mwaka 2017 baada ya miaka 39 tangu waliposhiriki mara ya mwisho mwaka 1978.  
    Mwaka 2017 Uganda haikushinda mechi hata moja AFCON katika Kundi D wakiambulia tu sare ya 1-1 na Benin baada ya kufungwa 1-0 na Ghana na Misri.
    Lakini mwaka huu ikishiriki fainali hizo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kujifunza kutokana na makosa ya 2017, tayari ina pointi nne baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya DRC na sare ya 1-1 na Zimbabwe na leo inaingia kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi A dhidi ya Misri kupigania tiketi ya hatua ya 16 Bora.
    Ni matarajio kabisa kurejea kwa Taifa Stars AFCON mwaka huu ni mwanzo mpya katika soka ya Tanzania na ni vyema tukajivunia hatua hiyo na kuungana pamoja kama nchi – pamoja na mapungufu yetu, kujipanga ili kwanza tuhakikishe tunafuzu na fainali zijazo.
    Taifa Stars imepitia mikononi mwa makocha na viongozi wengi, wachezaji wengi ambao wengi wetu leo tunawataja kama walikuwa bora kuliko wa sasa – lakini kwa miaka 39 haikufuzu AFCON.
    Inawezekana kuna makosa kweli kwenye benchi la Ufundi, wachezaji na hata kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) au Kamati ya Taifa Stars – lakini yanaweza yakawa chachu nzuri ya kujifunza.
    Ambavyo nchi yetu ina mapungufu ya watu wenye fikra na maono ya kimichezo, eti baada ya Taifa Stars kufungwa mechi ya kwanza tu, tena na Senegal kundi la Wabunge likiongozwa na Spika Job Ndugai likarejea nyumbani huku wakibeza kiwango cha timu – baadhi yao wamewahi kuwa viongozi wa klabu na Wizara za Michezo. Inasikitisha.
    Senegal ina wachezaji wenye uwezo mkubwa na wanaocheza Ulaya watupu, ambao wana uzoefu mkubwa wa mashindano makubwa wakiwa wanashika nafasi ya 22 katika renki za FIFA, ikiwa timu bora zaidi kundini, ikifuatiwa na Algeria ya 68, Kenya ya 105 na sisi (Tanzania) wa 131 inatufunga 2-0 tunavurugana? Kweli! Wabunge wetu walijishusha sana hapa.
    Tulitegemea Wabunge wangeshikamana na wachezaji na kuwatia moyo kuelekea mchezo uliofuata – badala yake wakahitimisha mashindano kwa maoni yao ambayo hayakuwa ya kitaalamu. Wenzetu wapo juu, sisi ndiyo tunapigana kupanda juu, hii ni safari inayohitaji ustahmilifu na mshikamano wa hali ya juu.
    Wakati umefika siasa na itikadi zake visiruhusiwe sana kuingilia michezo – ili kuepuka kuvuruga mambo na kuvurugana pia, kwani kwa wenye kujua soka Taifa Stars kufuzu tena AFCON baada ya miaka 39 ni ushindi mkubwa na kwa matokeo yoyote kwenye Fainali za mwaka huu nchini Misri ni fundisho na somo zuri kwetu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIASA NA ITIKADI ZAKE VISIRUHUSIWE SANA KUINGILIA KWENYE MICHEZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top