• HABARI MPYA

    Tuesday, June 25, 2019

    AMUNIKE ANA MATUMAINI YA KUIPIGA KENYA MECHI YA PILI YA AFCON ALHAMISI CAIRO

    Na Mwandishi Wetu, CAIRO
    KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania Taifa Stars, Emmanuel Amunike ana matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo wa pili wa mashindano ya Mataifa Afrika (AFCON)  dhidi ya Kenya katika mchezo utakaofanyika Juni 27 Uwanja wa 30 Juni mjini Cairo, Misri.
    Akizungumza na waandishi wa habari,Amunike,alisema anatambua Kenya ni timu nzuri na ina wachezaji wazuri,lakini hilo halimpi shida kwakuwa viwango vya wachezaji wa Kenya na vya wachezaji wa Tanzania  vinalingana, hivyo hana wasiwasi wa kupata matokea katika mchezo huo.
    “Timu zote ni za kutoka Afrika Mashariki na Kenya ni majirani zetu,na wote tunazungumza lugha ya Kiswahili, kwa hiyo hakuna kitu cha kujificha kitu kikubwa ni kwamba ni kwa jinsi gani tutaweza kufanya katika huo mchezo,tulionao  katika mchezo wa Senegal wachezaji walikuwa na uoga, lakini siwezi kuwalaumu, kwakuwa haya ni mashindano yao makubwa kucheza,” alisema na kuongeza:
    “Kitu kikubwa cha muhimu ambacho tunachokifanya kwasasa ni kuwapa moyo kuwajenga kiakili na kuwajengea ubora zaidi uwanjani wachezaji  kabla ya mchezo wetu unaofuata,binafsi  nina wachezaji bora na wenye uwezo,kwahiyo katika soka la kisasa naamini wanasifa za kushindana.”

    Emmanuel Amunike ana matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo dhidi ya Kenya keshokutwa

    Taifa Stars,inatarajia kushuka dimbani Alhamisi wiki hii, ikiwa na matumaini ya kupata alama tatu muhimu, ambazo zitaisaidia kuiweka katika mazingira mazuri ya kuweza kupata nafasi ya kufuzu kwa raundi ya pili ya mashindano.
    Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TFF, Mohammed Abdulaziz amewahakikishia wachezaji kuwa wajumbe wa kamati ya utendaji pamoja na Baraza la Wadhamini wapo pamoja nao, licha ya matokeo waliyoyapata katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Senegal.
    “Kwa upande wetu sisi, viongozi, tuna imani kubwa sana na kikosi chetu,licha ya matokeo ya jana, ambayo hayakuwa mazuri, lakini bado nasisitiza kuwa nafasi ipo na msivunjike moyo, hata nikitazama sura zenu bado napata matumaini kuwa tutafanya vyema katika michezo miwili iliyobakia.” alisema.
    Kwa upande wa nahodha wa timu ya Taifa Taifa Stars, Mbwana Samatta, aliwashukuru  viongozi hao wa kamati ya utendaji,Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini na Raisi wa TFF,Wallace Karia, kwa kuja kuwatembelea kambini na kuwatia moyo kuelekea michezo inayofuata dhidi ya Kenya na Algeria.
    Taifa stars,inatarajia kutupa karata yake ya pili katika mashindano ya Mataifa Afrika Juni 27,katika dimba la 30 June,kwa kucheza na Kenya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AMUNIKE ANA MATUMAINI YA KUIPIGA KENYA MECHI YA PILI YA AFCON ALHAMISI CAIRO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top