• HABARI MPYA

    Wednesday, June 26, 2019

    CLATOUS CHAMA ASAINI MKATABA MPYA WA MIAKA MIWILI KUENDELEA NA KAZI SIMBA SC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIUNGO Mzambia, Clatous Chota Chama maarufu kwa majina ya utani ya Triple C na Mwamba wa Lusaka, amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuichezea klabu ya Simba SC.
    Taarifa ya Simba SC mchana wa leo imesema kwamba baada ya kazi nzuri katika msimu wake wa kwanza, klabu imeridhika kumuongezea mkataba Chama.
    “Mfungaji wa magoli ya mwisho ambayo yalitupeleka kwenye hatua ya makundi na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Clatous Chota Chama (Triple C) bado yupo sana Msimbazi. Mwamba wa Lusaka ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Mabingwa baada ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili,”imesema taarifa ya Simba SC. 
    Clatous Chota Chama amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea na kazi Simba SC

    Chama anaingia kwenye orodha ya wachezaji wengine muhimu walioongeza mikataba chini ya kipa Aishi Manula, mabeki Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Nahodha Msaidizi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala, kiungo Jonas Mkude na washambuliaji Nahodha Mkuu, John Bocco na Meddie Kagere raia wa Rwanda.
    Na hiyo ni baada ya kazi nzuri msimu huu kwa pamoja na wenzao wakiiwezesha klabu kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na kufika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako walitolewa na vigogo, TP Mazembe ya DRC.
    Pamoja na kuwaongezea mikataba wachezaji wake wa msimu uliopita, Simba SC pia imesaini wachezaji wapya watano ambao ni kipa Beno Kakolanya kutoka Yanga, beki Kennedy Wilson Juma kutoka Singida United za nyumbani, kiungo Msudan, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman na Wabrazil, beki Gerson Fraga Vieira na mshambuliaji Wilker Henrique da Silva.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CLATOUS CHAMA ASAINI MKATABA MPYA WA MIAKA MIWILI KUENDELEA NA KAZI SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top