• HABARI MPYA

    Tuesday, June 25, 2019

    BEKI MBRAZIL ALIYECHEZA PAMOJA NA NEYMAR, PHILIPPE COUTINHO ASAINI MIAKA MIWILI SIMBA SC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BEKI wa kati na kiungo mkabaji, Mbrazil Gerson Fraga Vieira amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba SC.
    Vieira mwenye umri wa miaka 26 ametambulishwa leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu, Zacharia Hans Poppe na anajiunga na Wekundu wa Msimbazi akitokea klabu ya ATK ya India baada ya kumaliza mkataba wake.  
    “Fraga ambaye amewahi kuwa nahodha wa timu ya Taifa ya wachezaji chini ya miaka 17 ya Brazil iliyokuwa na wachezaji maarufu kama Neymar, Philippe Coutinho, Casemiro na golikipa Alisson, pia alicheza timu ya Taifa ya wachezaji chini ya miaka 20 na alicheza klabu kadhaa za Brazil ikiwepo Grêmio amejiunga na klabu yetu akitokea ATK FC ya India,”imesema taarifa ya Simba leo.
    Beki Mbrazil, Gerson Fraga Vieira (kulia) akisaini fomu za mkataba wa kujiunga na Simba pembeni ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu, Zacharia Hans Poppe  
    Zacharia Hans Poppe akipeana mkono na Gerson Fraga Vieira baada ya kusaini mkataba wa kujiunga na Simba 

    Gerson Fraga Vieira (wa tatu kulia waliosimama) akiwa kwenye kikosi cha timu ya vijana ya Brazil pamoja na Neymar wa PSG na Philippe Coutinho wa Barcelona

    Gerson Fraga mzaliwa wa Porto Alegre nchini Brazil, kisoka aliibukia timu ya vijana ya Gremio mwaka 2000 ambayo aliichezea hadi mwaka 2012 alipopandishwa timu ya wakubwa na akadumu hadi 2016.
    Lakini kwa sababu mbalimbali, akiwa Gremio alitiolewa kwa mkopo timu mbalimbali zikiwemo Oeste (2012), Red Bull Brasil (2014), Atenas (2014–2015), Red Bull Brasil (2015–2016) kabla ya kuuzwa moja kwa moja Mumbai City ya India mwaka 2016.
    Mwaka 2017 alihamia Atletico Tubarao alikocheza mechi 14 na kufunga bao moja kabla ya kurejea Mumbai City alikocheza hadi mwaka jana akahamia Renofa Yamaguchi ambako baada ya muda mfupi, akaondoka pia.
    Vieira ambaye pia amechezea pia timu za taifa za vijana za Brazil chini ya umri wa mkiaka 15 (U15) na U17, Renofa Yamaguchi alicheza mechi nne tu akahamia ATK alikocheza mechi 13 na kufunga bao moja pia kabla ya kuja kujaribu bahati yake Simba.
    Pamoja na Viera, Simba SC iko mbioni kumsajili mshambuliaji Ryan Moon kutoka Kaizer Chiefs ya kwao, Afrika Kusini ambaye naye amemaliza mikataba na klabu yake.
    Moon mwenye umri wa miaka 22, mzaliwa wa Pietermaritzburg, KwaZulu-Natal, Afrika Kusini baada ya kufanya vizuri na timu ya Maritzburg United aliyojiunga nayo akitoka kuzichezea Woodlands FC na Pirates FC, alipandishwa timu ya wakubwa mwaka 2016.
    Baada ya hapo alihamia Kaizer Chiefs mwaka 2016 ambako alidumu hadi mwishoni mwa msimu alipoachwa na sasa anakuja kujaribu bahati yake Simba SC.
    Amewahi pia kuchezea timu ya taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ kuanzia mwaka 2017 kwa mechi nane na kufunga bao moja tu.
    Fraga anakuwa mchezaji mpya wa tano kusajiliwa na Simba msimu huu baada ya kipa Beno Kakolanya kutoka Yanga, beki wa kati, Kennedy Wilson Juma kutoka Singida United wote Watanzania, kiungo wa kimataifa wa Sudan, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman na mshambuliaji Mbrazil, Wilker Henrique da Silva kutoka Bragantino ya Daraja la Nne nchini kwao.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BEKI MBRAZIL ALIYECHEZA PAMOJA NA NEYMAR, PHILIPPE COUTINHO ASAINI MIAKA MIWILI SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top