• HABARI MPYA

    Thursday, June 27, 2019

    SHOMARI KAPOMBE AONGEZA MKATABA MPYA WA MIAKA MIWILI KUBAKI SIMBA SC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BEKI wa kulia kimataifa wa Tanzania, Shomari Kapombe amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuichezea klabu ya Simba SC. 
    Taarifa ya Simba SC leo imesema kwamba Kapombe ambaye hajacheza mpira tangu Novemba mwaka jana alipoumia ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi baada ya kusaini mkataba huo.
    “Beki bora wa kulia nchini Shomari Kapombe amesaini mkataba mpya wa miaka miwili ambao utamwezesha kuendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Mabingwa. Shomari kwa sasa yupo fiti kucheza na atakuwa sehemu ya kikosi ambacho kitaenda nje ya nchi kujiandaa na msimu mpya,” imesema taarifa ya Simba leo.
    Shomari Kapombe amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuichezea klabu ya Simba SC

    Kapombe anaingia kwenye orodha ya wachezaji wengine waliokuwemo kwenye kikosi cha msimu uliopita cha Simba kusaini mkataba mpya.
    Wengine ni kipa Aishi Manula, mabeki Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Nahodha Msaidizi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala, viungo Jonas Mkude, Mzambia Clatous Chama na washambuliaji Nahodha Mkuu, John Bocco na Meddie Kagere raia wa Rwanda.
    Na hiyo ni baada ya kazi nzuri msimu huu kwa pamoja na wenzao wakiiwezesha klabu kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na kufika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako walitolewa na vigogo, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Pamoja na kuwaongezea mikataba wachezaji wake wa msimu uliopita, Simba SC pia imesaini wachezaji wapya watano ambao ni kipa Beno Kakolanya kutoka Yanga, beki Kennedy Wilson Juma kutoka Singida United za nyumbani, kiungo Msudan, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman na Wabrazil, beki Gerson Fraga Vieira na mshambuliaji Wilker Henrique da Silva.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SHOMARI KAPOMBE AONGEZA MKATABA MPYA WA MIAKA MIWILI KUBAKI SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top