• HABARI MPYA

    Wednesday, June 12, 2019

    AMUNIKE AWATEMA KICHUYA, BANDA, CHILUNDA NA MBAPPE KIKOSI CHA TAIFA STARS AFCON

    Na Mwandishi Wetu, ALEXANDRIA
    KOCHA Mnigeria Emmanuel Amunike amewachuja beki Abdi Hassan Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini na kiungo Shiza Ramadhani Kichuya anayecheza ENNPI kwa mkopo kutoka Pharco zote za Misri kwenye kikosi Tanzania ‘Taifa Stars’, kitakachoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zikazofanyika baadaye mwezi huu nchini Misri. 
    Baada ya kikao kizito leo mjini Alexandria ambako Taifa Stars imeweka kambi, hatimaye Amunike, winga wa zamani wa Barcelona ya Hispania na Super Eagles ametaja majina 23 ya kikosi chake cha AFON wengine aliowaengua ni pamoja na mshambuliaji Shaaban Iddi Chilunda anayecheza CD Izara kwa mkopo kutoka Tenerife, zote za Hispania.
    Wengine walioenguliwa ni kipa Suleiman Salula Malindi SC ya Zanzibar, mabeki Claryo Boniface wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes na David Mwantika wa Azam FC, kiungo Freddy Tangalu wa Lipuli FC na washambuliaji Miraj Athumani wa Lipuli FC na kinda wa Serengeti Boys (U17), Kelvin John ‘Mbappe’.

    Abdi Banda (wa pili kulia) ameenguliwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kitakachocheza AFCON 

    Kikosi kamili cha Taifa Stars kwa ajili ya AFCON kinaundwa na makipa; Aishi Manula (Simba SC), Metacha Mnata (Mbao FC) na Aaron Lulambo (Tanzania Prisons).
    Mabeki; Hassan Kessy (Nkana FC, Zambia), Vincent Philipo (Mbao FC), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni (Simba SC), Kelvin Yondan, Gardiel Michael (Yanga SC), Ally Mtoni (Lipuli FC) na Aggrey Morris (Azam FC).
    Viungo ni Feisal Salum (Yanga SC), Himid Mao (Petrojet, Misri), Frank Domayo, Mudathir Yahya (Azam FC), Simon Msuva (Difaa Hassan El-Jadidi Morocco) na Farid Mussa (Tenerife, Hispania).
    Washambuliaji ni Yahya Zayd (Ismailia, Misri), Rashid Mandawa (BDF, Botswana), Abdillah Abdallah Mussa, ‘Adi Yussuf’ (Blackpool, England), John Bocco (Simba SC), Thomas Ulimwengu (JS Saoura, Algeria) na Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji).  
    Benchi la Ufundi linaundwa na Amunike (Kocha Mkuu), Hemed Morocco (Kocha Msaidizi), Abelrahman Essa (Kocha wa Fiziki), Ali Taha (Mtathmini Mechi), Emeka Amadi (Kocha wa Makipa), Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa Ally Ruvu na Msaidizi wake, John Mashaka na Matabibu Dk Emil Richard Urasa, Dk Gilbert Kigadya na Dk. Richard Yomba.
    Taifa Stars itaanza na mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji wa AFCON, Misri Juni 13, mwaka huu Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria kabla ya kucheza mechi zake tatu za Kundi C mfululizo dhidi ya Senegal Juni 23, Kenya Juni 27 na Algeria Julai 1 kisha kuangalia matokeo yake kama yataipeleka hatua ya mtoano.  
    Mbali na Taifa Stars kupangwa Kundi C AFCON 2019 pamoja na jirani zao, Kenya, Algeria na Senegal – wenyeji, Misri wapo Kundi A pamoja na na Zimbabwe, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Kundi B linaundwa na Burundi, Madagascar, Guinea na Nigeria, Kundi D linaundwa na Namibia, Afrika Kusini, Ivory Coast na Morocco, wakati Kundi E kuna Angola, Mauritania, Mali na Tunisia na Kundi F ni Guinea Bessau, Benin, Ghana na mabingwa watetezi, Cameroon. 
    Taifa Stars imefuzu AFCON ya mwaka huu baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi L kwa pointi zake nane, nyuma ya jirani zao wa Afrika Mashariki, Uganda walioongoza kwa pointi zao 13 wakizipiku Lesotho iliyomaliza na pointi sita na Cape Verde pointi tano.    
    Mwaka huu, Tanzania itashiriki AFCON kwa mara ya pili tu kihistoria baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilipangwa Kundi A pamoja na wenyeji, Nigeria, Misri na Ivory Coast na kushika mkia.
    Mwaka 1980 ilifungwa mechi mbili, 3-1 na Nigeria na 2-1 na Misri kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Ivory Coast na kuishia Raundi ya kwanza tu, wakati timu nane tu zinashiriki michuano hiyo.   
    Michuano itaanza Juni 21 hadi Julai 19 na Taifa Stars itachezea mechi zake Uwanja wa Juni 30 na Al Salam mjini Cairo.
    Na katika CHAN, Taifa Stars itaanzia nyumbani dhidi ya Sudan Julai 26 kabla ya kurudiana Agosti 2 na ikifuzu mtihani huo itamenyana na mshindi kati ya Kenya na Burundi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AMUNIKE AWATEMA KICHUYA, BANDA, CHILUNDA NA MBAPPE KIKOSI CHA TAIFA STARS AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top