• HABARI MPYA

    Friday, September 12, 2014

    MAXIMO BADO KUMTOA COUTINHO YANGA NA AZAM KESHO TAIFA, AMPA HADI KESHO JIONI

    Na Nagma Khalid, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Mbrazil Marcio Maximo amesema kesho jioni ndiyo atajua kama kiungo wake, Andrey Coutinho anaweza kucheza au kutocheza mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam mchana wa leo, Maximo amesema hadi sasa, Mbrazil mwenzake huyo ana asilimia sawa za kucheza na kutocheza Jumapili. 
    Kiungo huyo Mbrazil aliumia katika mchezo wa kirafiki asubuhi ya juzi dhidi ya Polisi ya Dar es Salaam Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibio, Dar es Salaam.
    Andrey Coutinho anaweza kucheza au kutocheza Jumapili baada ya kuumia juzi

    Coutinho ambaye jana jioni alifanya mazoezi ya viungo gym, alikuwa anajaribu kugeuka apige mpira juzi Loyola, akateguka kifundo cha mguu na kushindwa kuendelea na mchezo uliomalizika kwa sare ya 0-0.
    Maximo amesema mshambuliaji Jerry Tegete hawezi kabisa kushiriki mchezo huo kwa sababu anasumbuliwa na maumivu ya nyonga.
    Hata hivyo, kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars amesema kwamba mshambuliaji Hamisi Kiiza amerejea jana kutoka Uganda ambako alikwenda kuichezea timu yake ya taifa, The Cranes na moja kwa moja anaingia kwenye programu ya mchezo wa keshokutwa, ambao atatumia mfumo wa 4-4-2. 
    Amesema anawajua Azam FC na anawaheshimu, kwani ni timu bora ambayo imekuja kubadilishia soka ya Tanzania. Maximo amesema wachezaji wake wapo tayari sana kwa ajili ya mechi hiyo na kwamba mechi za kujipima walizocheza zimemsaidia kwa kiasi kikubwa.
    Amewataka wapenzi na mashabiki wa Yanga SC kujitokeza kwa wingi kesho kuisapoti timu hiyo ili ishinde. “Pamoja tunaweza,”alisema Maximo kwa Kiswahili.
    Yanga SC ndio washindi mara nyingi zaidi wa Ngao, mara ya kwanza wakitwaa mwaka 2001 walipoifunga mabao 2-1 Simba SC, enzi hizo Ligi Kuu inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager. 
    Baada ya hapo, haikuchezwa tena mechi ya Ngao hadi mwaka 2009 wakati Mtibwa Sugar ilipoilaza 1-0 Yanga SC.
    Mwaka 2010 Yanga walirejesha Ngao kwenye himaya yao, baada ya kuwachapa tena wapinzani wao wa jadi, Simba kwa penalti 3-1 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90.
    Simba SC walitwaa mara mbili mfululizo Ngao na kufikia rekodi ya watani, kwanza 2011 walipoifunga 2-0 Yanga na 2012 walipotoka nyuma kwa 2-0 na kuilaza Azam 3-2.
    Mwaka jana, Yanga SC ikaweka rekodi ya kuwa timu iliyotwaa mara nyingi zaidi Ngao ya Jamii, baada ya kuilaza 1-0 Azam FC, bao pekee la kiungo Salum Abdul Telela ‘Master’.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAXIMO BADO KUMTOA COUTINHO YANGA NA AZAM KESHO TAIFA, AMPA HADI KESHO JIONI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top