• HABARI MPYA

    Friday, September 12, 2014

    MBEYA CITY KUCHEZA NA WAKALI WA UGANDA JUMAMOSI SOKOINE

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    MBEYA City itashuka dimbani kesho kwenye Uwanja wa Sokoine kumenyana na Vipers FC, zamani Bunamwaya FC ya Uganda katika mchezo wa kirafiki.
    Mchezo huo wa mwisho wa kujipima nguvu kwa Mbeya City kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara unatarajiwa kuanza Saa 10:00 jioni na kiingilio kitakuwa Sh. 3,000.
    Ofisa Habari wa MCC, Dismas Ten ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba kocha Juma Mwambusi anataka kuutumia mchezo huo kukipima kikosi chake kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu wiki ijayo.
    Mbeya City watacheza mchezo wa kujipima nguvu na Vipers ya Uganda kesho

    Ligi Kuu inatarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu na Mbeya City watafungua dimba na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Sokoine siku hiyo.
    Mabingwa watetezi, Azam FC watafungua dimba na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, wakati washindi wa pili 
    Yanga SC wataanza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro siku hiyo.
    Mechi nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu zitakuwa kati ya Stand United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
    Mabingwa wa zamani wa ligi hiyo, Simba SC wataanza kampeni ya kutwaa tena taji hilo Septemba 21 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ligi hiyo itatanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii utakaochezwa keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Azam FC na Yanga SC. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBEYA CITY KUCHEZA NA WAKALI WA UGANDA JUMAMOSI SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top