• HABARI MPYA

    Friday, September 12, 2014

    AZAM NA YANGA KILA KITU KITASUBIRI JUMAPILI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    GUMZO kubwa katika soka ya Tanzania hivi sasa ni Yanga na Azam. Hao ndiyo waliokuwa washindani wa taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa misimu iliyopita na wamepokezana taji ndani ya miaka hiyo miwili.
    Alianza Azam FC kurithi taji lililotemwa na Simba msimu wa 2012/2013 na Yanga SC wakafuatia msimu uliopita 2013/2014.
    Pazia la Ligi Kuu msimu mpya wa 2014/2015 linafunguliwa Jumapili kwa mchezo wa Ngao ya Jamii, baina ya mabingwa Azam FC dhidi ya Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Azam FC walikuwa mabingwa msimu uliopita, lakini ukweli usiopingika Yanga SC walikuwa wana timu bora zaidi, ila kushindwa kuchanga karata zao vyema katika mechi za mwishoni kuliwaangusha.
    Jumapili tena; Hamisi Kiiza wa Yanga SC akiwatoka mabeki wa Azam FC, David Mwantika na Erasto Nyoni nyuma msimu uliopita. Timu hizo zinakutana keshokutwa Uwanja wa Taifa 

    Ndiyo maana, baada ya msimu ni Azam FC walioingia sokoni na mamilioni kuboresha kikosi, wakibeba nyota wawili wa wapinzani wao hao, kiungo Frank Domayo na mshambuliaji Didier Kavumbangu.
    Ilibaki kidogo tu na Athumani Iddi ‘Chuji’ asajiliwe Azam FC kama si msimamo mkali wa mmoja wa Wakurugenzi wa timu hiyo, aliyepinga mchezaji huyo kusajiliwa. Chuji amekwenda Oman.
    Mbali na kuchukua nyota wawili wa Jangwani, Azam FC imesajili pia wachezaji wengine wawili wa kigeni, washambuliaji Ismaila Diara kutoka Mali na Leonel Saint- Preux kutoka Haiti pamoja na beki Mtanzania, Shomary Kapombe aliyekuwa AS Cannes ya Ufaransa.
    Frank Domayo ni majeruhi na labda ataanza kucheza mwakani, lakini kikosi cha Azam FC kina wachezaji watatu wapya wa maana, Kapombe, Leonel na Kavumbangu.
    Bado wakali wawili wa Ivory Coast, pacha Kipre Tchetche na Kipre Balou wapo kikosini- sambamba na nyota wote wa kikosi hicho kwa miaka kadhaa kama Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Khamis Mcha ‘Vialli’, Eradto Nyoni, Aggrey Morris na wengine unaowajua.     
    Diara hana nafasi kikosi cha kwanza mbele ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog na huwezi kusita kuuita ulikuwa usajili mbovu- lakini kwa Kapombe, Leonel na Kavumbangu, Azam FC imeboresha kikosi.
    Imeingiza askari watatu wa maana wanaoimarisha mapambano ya utawala wa soka ya Tanzania na kuelekea mchezo wa Jumapili imani ni kubwa mno upande wa timu hiyo inayomilikiwa na Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake. 

    ZILIPOKUTANA MARA YA MWISHO YANGA NA AZAM: 

    MACHI 19, 2014, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
    BAO la dakika ya 83 la kinda Kevin Friday limeinusuru Azam FC kulala mbele ya Yanga SC baada ya kulazimisha sare ya kufungana 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Azam ilicheza kwa zaidi ya dakika 20 za mwisho ikiwa pungufu baada ya beki wake wa kulia, Erasto Nyoni kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kutoa lugha chafu kwa refa. 
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa askari wa jeshi la Polisi Tanzania, Hashim Abdallah wa Dar es Salaam aliyesaidiwa na Anold Bugado wa Singida na Florentina Zablon wa Dodoma, hadi mapumziko tayari Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.
    Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji kutoka Burundi, Didier Kavumbangu dakika ya 14 aliyekutana na mpira uliorudi baada ya kupanguliwa na kipa Aishi Salum Manula kufuatia kutokea piga nikupige langoni mwa Azam. 
    Shambulizi lililozaa bao hilo lilianzia kwa kwa Simon Msuva aliyemtoka beki Gadiel Michael wingi ya kulia na kutia krosi iliyounganishwa na Kavumbangu lakini mpira ukagonga mwamba na kurudi uwanjani na kumkuta Hamisi Kiiza aliyepiga kipa akaokoa na kumkuta mfungaji aliyemaliza kazi.
    Azam FC ilikosa mabao mawili ya wazi kipindi cha kwanza, wakati bao lililofungwa na Kipre Herman Tchetche refa Hashim alikataa kwa sababu mpigaji kabla ya kufumua shuti alimsukuma beki Kevin Yondan.  
    Wachezaji wa Azam mara mbili walimfuata refa Hashim kumlalamikia kwa kutoridhishwa na uamuzi wake, mfano alipokataa bao na mara moja alipokataa kutoa mpira wa adhabu baada ya John Bocco kuangushwa karibu na eneo la hatari.
    Kipindi cha pili timu zote ziliingia na vikosi vile vile, Azam wakiendelea kusaka bao la kusawazisha na Yanga wakitaka kunenepesha ushindi wao.
    Hata hivyo, nyota ya Yanga SC iliendelea kung’ara baada ya kupata penalti dakika ya 69 kufuatia beki Said Mourad ‘Mweda’ kuunawa mpira uliopigwa na Didier Kavumbangu, hata hivyo mkwaju wa Hamisi Kiiza ‘Diego’ ulipanguliwa vizuri na kipa Aishi Salum Manula na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda. 
    Baada ya kona hiyo wachezaji wa Azam wa Azam FC walikwenda kumlalamikia refa ambaye alimuonyesha kadi ya pili ya njano Erasto Nyoni na kuwa nyekundu.
    Pamoja na kubaki wachache, Azam waliendelea na jitihada za kusaka bao la kusawazisha na dakika ya 83 kinda aliyepandishwa kutoka kikosi cha pili, Kevin Friday aliipokea vyema pasi ya Salum Abubakr ‘Sure Boy’ na kumchambua kipa mkongwe Juma Kaseja.
    Kelvin Friday aliifungia Azam FC bao la kusawazisha dakika za lala salama
    Kutoka hapo Azam walicharuka zaidi na kufanya mashambulizi mawili zaidi, lakini hawakufanikiwa kupata bao.

    Kwa ujumla mchezo ulikuwa mkali na wa ushindani- wenye hadhi ya Ligi Kuu kweli. Azam FC sasa inajiongezea pointi moja na kufikisha pointi 44 baada ya mechi 20, wakati Yanga SC inatimiza pointi 40 baada ya mechi 19.  
    Yanga SC; Juma Kaseja, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Didier Kavumbangu/Mrisho Ngassa dk73, Hamisi Kiiza/Hussein Javu dk87 na Emmanuel Okwi.
    Azam FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Said Mourad, Kipre Balou, Himid Mao, Salum Abubakar, John Bocco, Kipre Tchetche na Khamis Mcha/Kevin Friday dk49.
    Mtu hatari; Kipre Tchetche wa Azam FC kulia akitafuta mbinu za kumtoka Kevin Yondan wa Yanga SC

    REKODI YA YANGA NA AZM FC LIGI KUU: 

    Machi 19, 2014; 
    Yanga SC 1-1 Azam FC
    Septemba 22, 2013; 
    Azam FC 3-2 Yanga SC
    Februari 23, 2013;  
    Yanga SC 1-0 Azam FC (Ngao ya Jamii)
    Novemba 4, 2012;  
    Azam FC 0-2 Yanga SC
    Machi 10, 2012; 
    Yanga SC 1-3 Azam FC
    Septemba 18, 2011;  
    Azam 1-0 Yanga SC
    Machi 30, 2011;  
    Yanga SC 2-1 Azam FC
    Oktoba 24, 2010; 
    Azam FC 0-0 Yanga SC
    Machi  7, 2010;  
    Yanga SC 2-1 Azam FC   
    Oktoba 17, 2009; 
    Azam FC 1-1 Yanga SC
    Aprili 8, 2009;  
    Yanga SC 2-3 Azam FC
    Oktoba 15, 2008;  
    Azam FC 1-3 Yanga SC

    Msimu uliopita, Azam FC na Yanga SC zilitambiana sawa- kwani katika mechi tatu kila timu ilishinda mechi moja na mchezo mmoja wakatoka sare, ingawa Yanga SC ilikuwa katika nafasi ya kushinda mechi zote.

    Yanga SC ilishinda mechi ya Ngao ya Jamii 1-0 na mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Azam FC ikatoka nyuma kwa 2-1 na kushinda 3-2 dakika za lala salama.
    Mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu, Azam FC ilisawazisha dakika za mwishoni kupata sare ya 1-1 katika mchezo ambao kipa Aishi Manula alicheza penalti ya Hamisi Kiiza ‘Diego’.
    Historia ya Azam FC na Yanga SC itaendelea Jumapili na je, ni nani atakayeuanza msimu kwa kumtambia mwenzake?
    Mechi ya Ngao ni lazima mshindi apatikane, kwani kama matokeo yatakuwa sare, mikwaju ya penalti itaamua mtu wa kubebeshwa ‘Ubao’.   

    MECHI YA KUKUMBUKWA YANGA NA AZAM FC: 

    Machi 10, 2012; Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam 
    Yanga SC na Azam FC zimekutana mara 11 katika mechi za Ligi Kuu na mara moja katika mechi ya Ngao ya Jamii, jumla mara 12 katika mechi za mashindano ya mataji Bara.
    Sahau kuhusu mechi za kirafiki na vikombe kama Mapinduzi na Kagame- katika mechi za Ligi Kuu, kila timu imeshinda mara nne, wakati tatu wametoka sare na Yanga ilishinda mechi moja ya Ngao waliyokutana hadi sasa.
    Mechi moja tu itabaki kuwa ya kihistoria baina ya timu hizo- ile ya Machi 10, mwaka 2012 ambayo ilikuwa mzunguko wa pili Ligi Kuu, iliyomalizika kwa Uwanja wa Taifa kugeuka eneo la mapambano baina ya Polisi na mashabiki wa Yanga. 
    Polisi walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki wa Yanga waliotaka kumpiga refa, wakifanya vurugu za kung’oa viti na kutupa ovyo uwanjani.
    Hiyo ilifuatia Yanga SC kufungwa 3-1, refa Israel Nkongo akitoa kadi nyekundu mbili kwa wachezaji Haruna Niyonzima na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
    Niyonzima alikuwa chanzo cha vurugu na baadaye beki Stefano Mwasyika akaenda kumtwanga ngumi refa huyo- kabla ya wachezaji wengine wa timu hiyo kumvaa Nkongo.
    Mchezo ulisimama kwa dakika kadhaa kupisha vurugu hizo na baada ya hapo, Nkongo akatoa kadi nyekundu kwa Niyonzima na Cananvaro. Mwasyika ambaye pamoja na kuonekana akirusha ngumi hakupewa kadi, baadaye alifungiwa mwaka mmoja na faini ya Sh Milioni 1, Jerry Tegete alifungiwa miezi sita na faini ya Sh. 500,000, Cannavaro alifungiwa mechi sita na faini ya Sh. 500, 000, Nurdin Bakari na Omega Seme walifungiwa mechi tatu na faini ya Sh. 500,000, wakati Yanga ilitozwa faini ya Sh Milioni 4.5. Haitarajiwi tena mechi baina ya timu hizo kufikia katika hatua hiyo.
    Wachezaji wa Yanga SC wakimfanyizia refa Israel Nkongo Machi 10, 2012 Uwanja wa Taifa 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM NA YANGA KILA KITU KITASUBIRI JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top