• HABARI MPYA

    Friday, September 12, 2014

    URA WAWASILI DAR KAMILI NA WAKALI WA THE CRANES, SHUGHULI WANAYO SIMBA SC TAIFA LEO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Mamlaka ya Mapato Uganda (URA) imewasili usiku wa jana tayari kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Simba SC jioni ya leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mabingwa hao wa zamani wa Uganda walichelewa kufika Dar es Salaam kutokana na kuwasubiri wachezaji wao waliokuwa timu ya taifa, Uganda The Cranes ambayo juzi ilifunga Guinea mabao 2-0 katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika mjini Kampala Jumapili.
    URA wamewasili na kikosi chao kamili na wapo tayari kutoa ushindani mkali kwa Wekundu wa Msimbazi, ambao hivi sasa wanaonekana kuwa imara baada ya kuyumba kwa misimu miwili iliyopita.   
    Wamewasili; Wachezaji wa URA baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) usiku wa jana


    Kocha Patrick Phiri anatarajiwa kuutumia mchezo wa leo utakaoanza Saa 11:00 jioni kukifanyia tathmini ya mwisho kikosi chake kabla ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuanza wiki ijayo.
    Makamu wa Rais wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ameiambia BIN ZUBEIRY asububi ya leo kwamba kikosi cha Simba SC kipo imara kambini Mbezi Beach kwa ajili ya mchezo huo na wapenzi watarajie burudani nzuri.
    “Kama nilivyosema awali, kwamba tumewaalika URA kwa sababu ni moja ya timu bora kabisa katika ukanda wetu huu na ina wachezaji wengi timu ya taifa ya Uganda ambayo inaendelea vizuri kwenye mechi za kufuzu AFCON,”.
    Kaburu amewaomba wapenzi wa Simba SC kote Dar es Salaam wajitokeze kwa wingi leo kuishuhudia timu yao kwa mara ya mwisho kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
    “Tulisema, lengo la mechi hii ni kuuthibitisha uwezo wa wachezaji wetu na timu yetu kwa ujumla kabla ya ligi kuanza, sasa tunaomba sana sana, wapenzi wote wa Simba SC waje kwa wingi ili kusudi tusaidiane kutazama ubora wa kikosi chetu,”amesema.
    Simba SC imecheza mechi nne chini ya Phiri za kujipima nguvu na kushinda zote, dhidi ya Kilimani FC 2-1, Mafunzo 2-0, KMKM 5-0 zote Zanzibar na Gor Mahia ya Kenya 3-0.
    Phiri alirithi mikoba ya Mcroatia, Zdravko Logarusic aliyetupiwa virago mwezi uliopita baada ya timu hiyo kufungwa mabao 3-0 na ZESCO United ya Zambia katika mchezo wa kirafiki Dar es Salaam. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: URA WAWASILI DAR KAMILI NA WAKALI WA THE CRANES, SHUGHULI WANAYO SIMBA SC TAIFA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top