Kikosi cha Stars |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
KOCHA wa
timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Mdenmark Kim Poulsen amesema hana
majeruhi hata mmoja kikosini mwake kuelekea mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la
Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kesho, Uwanja wa
Mandela, Namboole mjini hapa.
Akizungumza leo
mjini hapa baada ya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu Kyambogo, Poulsen
alisema kwamba timu iko tayari kwa mchezo huo wa kesho unaotarajiwa kuwa wa
kukata na shoka.
“Vijana
wamejiandaa vizuri kabisa na wote wako katika hali nzuri ya kucheza ila
tunachoomba ni fair play kutoka kwa muamuzi maana tunacheza na wenyeji ambao
wana watazamaji wengi,” alisema.
Alisema timu
zote mbili ni nzuri na iwapo muamuzi atachezesha vizuri basi utakuwa ni mchuano
mkali. “Vijana wana ari na mchezo huu na tukipewa fair play tutacheza vizuri
kama tulivyofanya katika michezo dhidi
ya Rwanda,” alisema Poulsen.
Refa wa
mechi ya Cranes na Stars anatarajiwa kuwa Mohamed El Fadil kutoka Sudan ambaye
pia alichezesha mechi ya Stars dhidi ya Rwanda Robo Fainali.
Alisema ana
furaha kwa kuwa hakuna majeruhi hata mmoja na pia aliwasifu wachezaji wake kwa
kuonyesha umoja na nidahmmu ya hali ya juu. “Hawa wanakaa kama familia si
unawaona walivyo pamoja?” alisema Poulsen na kuongeza kuwa hilo ni muhimu sana
kwa mchezaji.
Naye kocha
msaidizi, Sylvester Mash alisema Stars ina nafasi kubwa sana ya kushinda mechi
hii kwa sababu wenyeji wao, The Cranes watakuwa wanacheza kwa wasiwasi kwa kuwa
wako nyumbani .
“Timu yetu ina
hamasa kabisa na ukizingatia Uganda wako nyumbani, wao ndio wana tension kubwa
zaidi,” alisema na kuongeza kuwa mchezo huu utakuwa wa kusisimua sana.
Akizungumza
kutoka Dar es Salaam, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, wadhaminiwa
Stars, George Kavishe alisema Stars ina kila sababu ya kutinga fainali na kunyanyua
kombe kwa mara ya nne.
“Sisi kama
wadhamini tunasubiri ushindi maana tuna imani na Stars na hatua waliyofikia ni
nzuri nay a kutia moyo kwa hivyo watanzania wajitokeze kwa wingi na kuufuatilia
mchezo huu kesho,” alisema Kavishe.
Mchezo wa
Stars na Cranes utatanguliwa na semi fainali ya kwanza kati ya Zanzibar na
Kenya ambao pia ni mchezo wa kusisimua kwani timu zote mbili zimeshaonyesha
uwezo mkubwa.
Kocha wa
Zanzibar Salum Nassor ameshatangaza mara mbili akiwa Zanzibar na hapa Kampala
kuwa iwapo hataondoka na kombe basi atabwaga manyanga.