Simba |
VIKOSI:
SIMBA: Juma Kaseja, Nassor Chollo, Amir
Maftah, Shomary Kapombe, Kelvin Yondan, Patrick Mafisango, Uhuru Suleiman,
Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi na Emanuel Okwi.
BENCHI: Ally Barthez, Derrick Walullya, Obadia
Mungusa, Victor Costa, Ramadhan Singano, Gervais Kago na Salum Machaku.
Yanga |
YANGA: Yaw Berko, Nsajigwa Shadrack, Oscar
Joshua, Nadir Cannavaro, Athumani Iddi, Juma Seif, Shamte Ally, Haruna
Nironzima, Davies Mwape, Kenneth Asamoah na Hamisi Kiiza.
BENCHI: Shaaban Kado, Omega Seme, Zuberi Ubwa,
Job Ibrahim, Bakari Mbega, Nurdin Bakari, Idrisa Senga, Pius Kisambale na Geoffrey
Bonny.
WATANI wa jadi katika soka ya Tanzania,
Simba na Yanga wanashuka dimbani leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
katika mchezo wa funga dimba, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, huku kila timu
ikihitaji kulinda hadhi yake tu.
SImba tayari bingwa- lakini ili sherehe za
kukabidhiwa Kombe zinoge lazima wamfunge mtani wa jadi- lakini kwa Yanga, baada
ya kupokonywa ubingwa wa Bara na kukosa hata nafasi ya pili, kitu pekee cha
kuwafariji mashabiki wao ni kuua mnyama.
Yanga leo itamkosa mshambuliaji wake mzoefu
wa mechi za watani wa jadi, Jerry Tegete ambaye anatumikia adhabu ya kutocheza
hadi mwisho mwa msimu.
Simba inaingia kwenye mchezo wa leo ikiwa
katika mwendo mzuri- ikishinda mechi za ligi na za Afrika- zaidi safu yake ya
ushambuliaji inaonekana kuchanganya zaidi katika siku za karibuni.
Hapana shaka, Mserbia Milovan Cirkovick
ataendelea kuwapanga pamoja Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ na Felix Sunzu
katikati na pembeni yao Emmanuel Okwi kushoto na Uhuru Suleiman kulia- hii maana
yake atashambulia na wanaume wanne.
Yanga kadhalika- kuna uwezekano Freddy
Felix Minziro akatumia washambuliaji wanne- Kenneth Asamoah na Davies Mwape
katikati na pembeni yao Hamisi Kiiza kushoto na Shamte Ally kulia.
Haruna Niyonzima katika kiungo cha Yanga na
Mwinyi Kazimoto katika kiungo cha Simba ni burudani nzuri inayotarajiwa Taifa
leo.
Patrick Mafisango atacheza kama kiungo wa
ulinzi, lakini kwa sababu anapanda sana- inamaanisha Simba inawezaa kuifunika
Yanga katika nafasi ya kiungo- itategemea Juma Seif ‘Kijiko’ atakuwa katika
hali gani leo na atachezaje, maana jamaa huwa hatabiriki.
Beki wa kulia wa Yanga atakuwa ‘babu’
Nsajigwa Shadrack upande ule ambao atakuwa anateleza Okwi- wakati kulia
atakuwapo Oscar Joshua eneo ambalo ni njia ya Uhuru.
Beki wa kulia wa SImba bila shaka atakuwa
Nassor Masoud ‘Chollo’ ambako atakuwa anapita Kiiza na beki wa kushoto atakuwa
Amir Maftah katika njia ya Shamte Ally.
Katikati Yanga, Minziro anaweza kuamua kumpanga
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Chacha Marwa au kuendelea kumchezesha pamoja na
Athumani Iddi ‘Chuji’.
Simba hapana shaka Milovan ataendelea
kuwachezesha pamoja katikati Shomary Kapombe na Kelivn Yondan. Langoni Simba
piga, ua atasimama Kaseja tu labda awe mgonjwa wa kushindwa kucheza hata kwa
sindano ya ganzi. Yanga bila shaka atadaka Mghana Yawe Berko.
JE WAJUA?
Mara ya mwisho Simba na Yanga kukutana
katika mechi ya kulinda heshima- baada ya tayari kuwa bingwa amekwishapatikana
ilikuwa ni Aprili 27, mwaka 2008 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na timu hizo
zilitoka sare ya bila kufungana, Yanga ikiwa tayari imekwishatwaa ubingwa chini
ya kocha Mserbia Profesa Dusan Savo Kondic.
Kocha wa Simba katika mechi hiyo ya Aprili 27,
2008 alikuwa ni Profesa Milovan Cirkovic, ambaye baada ya mechi hiyo aliondoka
SImba kutokana na uongozi wa klabu hiyo, chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wake,
Hassan Daalal kugoma kumuongezea mshahara.
Pambano la kwanza la Ligi Kuu, wakati huo
klabu ya bingwa ya taifa baina ya watani wa jadi lilifanyika Juni 7, mwaka 1965
Uwanja wa Ilala (sasa Karume), wakati huo Simba bado inaitwa Sunderland na
Yanga ndio walioshinda mechi hiyo, bao pekee la
Mawazo Shomvi dakika ya 15.
Ushindi mkubwa zaidi kwa Yanga dhidi ya
watani wao wa jadi, Simba ni wa mabao 5-0 Juni 1, 1968, siku hiyo Maulid Dilunga
‘Mexico’ akifunga mabao mawili katika dakika ya 18 kwa penalti na na 43, wakati
mengine yalifungwa na Salehe Zimbwe dakika ya 54 na 89 na Kitwana Manara dakika
ya 86.
Simba ililipa kisasi cha 5-0 Julai 19,
mwaka 1977 kwa kuwafunga Yanga mabao 6-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam- siku
hiyo Abdallah ‘King’ Kibadeni akifunga mabao matatu peke yake katika dakika za
10, 42 na 89 wakati mengine yalifungwa na Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika ya
60 na 73 na beki wa Yanga, Suleiman Sanga akajifunga dakika ya 20.
Sare ya mabao 4-4 Novemba 9, mwaka 1996 Uwanja
wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, inabakia kuwa sare ya kihistoria katika
mapambano ya watani wa jadi kufungana mabao mengi. Mabao ya Yanga yalifungwa na
Edibilly Lunyamila kwa penalti dakika ya 28, Mustafa Hozza alijifunga dakika ya
64, Said Mwamba 'Kizota' dakika ya 70 na Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ dakika ya 75.
Simba mabao yao yalifungwa na Thomas Kipese dakika ya saba, Ahmed Mwinyimkuu dakika
ya 43 na Dua Saidi dakika ya 60 na 90.
Leo Yanga inatarajiwa kuongozwa na kocha
mzalendo, beki wake wa zamani Freddy Felix Minziro wakati Simba ina Mserbia,
Milovan Cirkovic- hii ni mara ya kwanza benchi la Yanga kuwa na kocha mzawa
katika mechi dhidi ya watani tangu alipofukuzwa Kenny Mwaisabula mwaka 2004.
Juma Kaseja atakuwa ni mchezaji aliyeanza
muda mrefu zaidi kucheza mechi za watani wa jadi, mwaka 2003 mechi yake ya
kwanza ikiwa ni ya Aprili 20, mwaka 2003 akikaribishwa na kipigo cha mabao 3-0,
yaliyotupiwa nyavuni na Kudra Omary dakika ya 30, Heri Morris dakika ya 32 na
Salum Athumani dakika ya 47.
Washambuliaji wote wa kigeni wa Yanga, Mghana
Kenneth Asamoah, Mganda Hamisi Kiiza na Mzambia Davies Mwape wamekwishatikisa nyavu
za Simba- ingawa bao la Kiiza lilikataliwa kwenye fainali ya Kombe la Kagame
Julai mwaka jana, kwa madai aliotea, lakini lilionekana kuwa bao salama kabisa.
Ni mshambuliaji mmoja tu wa kigeni wa
Simba, Felix Mumba Sunzu Jr katika washambuliaji watatu wa kigeni wa Simba, wengine
wakiwa Gervais Kago kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati na Emmanuel Okwi kutoka
Uganda aliyeweza kutikisa nyavu za Yanga.
Kiungo Patrick Mutesa Mafisango wa Simba
kutoka Rwanda, amekwishatikisa nyavu za Yanga katika msimu wake huu wa kwanza
Msimbazi- lakini Mnyarwanda mwenzake Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima anaingia
kwenye mechi ya mwisho ya msimu leo- akiwa hajui nyavu za SImba zinatikisikaje.
Hili linakuwa pambano la 11, kwa watani wa
jadi kukutana Uwanja mpya wa Taifa tangu ufunguliwe, awali katika mapambano 10,
Yanga ilishinda mechi tano, Oktoba 26, 2008 (1-0), Oktoba 29, 2011 (1-0), Julai
10, 2011 (1-0), Desemba 25, 2009 (2-1) na Agosti 18, 2010, iliposhindwa penalti
3-1 baadaye ya sare 0-0, wakati Simba imeshinda mechi tatu tu Oktoba 31, 2009 (1-0),
Aprili 18, 2010 (4-3) na Agosti 17, 2011 (2-0) na timu zimetoka sare mara mbili,
Aprili 19, 2009 (2-2) na Machi 5, 2011 (1-1).
Kiiza kushoto na Chollo kulia, leo itakuwaje? |
0 comments:
Post a Comment