• HABARI MPYA

    Thursday, May 03, 2012

    NGORONGORO WATUA SALAMA KHARTOUM TAYARI KUMALIZA KAZI KESHOKUTWA


    Tegemeo la Ngorongoro,
    Thomas Ulimwengu

    TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes imewasili salama hapa Khartoum jana saa 4 usiku kwa ajili ya mechi ya michuano ya
    Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 dhidi ya Sudan. Mechi hiyo itachezwa Jumamosi kuanzia
    saa 2.00 usiku kwenye Uwanja wa Khartoum ambao ni wa nyasi bandia, na hakutakuwa na kiingilio kwa
    watazamaji.
     
    Awali Ngorongoro Heroes ilitarajiwa kuwasili saa 2.10 usiku, lakini ndege iliyokuwa ipande Nairobi kuja
    hapa ilichelewa kuondoka kwa saa moja na nusu kutokana na hali ya hewa kutokuwa nzuri katika Uwanja
    wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kulikosababishwa na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha
    uwanjani hapo.
     
    Mara baada ya kuwasili Taka Hotel ambapo imefikia, Ngorongoro Heroes ilifanya mazoezi ya saa moja
    kuanzia saa 4.30 usiku kwenye Uwanja wa Khartoum ambao ndiyo utakaotumika kwa mechi dhidi ya
    Sudan. Ngorongoro Heroes ilishinda mchezo wa kwanza mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
    Salaam.
     
    Hoteli ya Taka ndipo pia timu ya El Merreikh ya hapa Sudan imeweka kambi yake kujiandaa kwa mechi ya
    marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
    El Merreikh ililala mabao 2-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Lubumbashi.
     
    Kwa mujibu wa kocha Kim Poulsen, wachezaji wote wako katika hali nzuri na kikosi kitakachoanza kwenye
    mechi hiyo kitajulikana kesho (Ijumaa) baada ya mazoezi ya mwisho yatakayofanyika saa 2 usiku kwenye
    Uwanja wa Khartoum.
     
    Wachezaji walioko kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes ni Aishi Manula, Ramadhan Singano, Hassan
    Dilunga, Frank Damayo, Frank Sekule, Issa Rashid, Hassan Ramadhan, Saleh Malande, Said Zege, Emily
    Mugeta, Jerome Lambele, Samir Ruhava, Simon Msuva, Thomas Ulimwengu, Atupele Green, Dizana
    Yarouk, Jamal Mroki na nahodha Omega Seme.
     
    Mwamuzi Aden Abdi Djamal wa Djibouti ndiye atakayechezesha mechi hiyo. Djamal atasaidiwa na
    Wadjibouti wenzake Egueh Yacin Hassan, Bogoreh Salime Fahan na Aden Ali Farah. Waamuzi hao
    watawasili kesho (Ijumaa) saa 8 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines wakati Kamishna wa mechi hiyo
    Patrick Naggi kutoka Kenya atawasili leo (Alhamisi) saa 2.10 usiku kwa ndege ya Kenya Airways.
     
    Iwapo Ngorongoro Heroes itafanikiwa kuitoa Sudan itacheza mechi ya raundi ya pili dhidi ya Nigeria. Mechi
    ya kwanza itchezwa Julai 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano itakuwa kati ya Agosti 10
    na 12 mwaka huu.
     
    Ikifanikiwa kuitoa Nigeria, Ngorongoro Heroes itacheza mechi ya raundi ya tatu na mshindi kati ya Afrika
    Kusini na Congo Brazzaville. Mechi ya kwanza itakuwa ugenini kati ya Septemba 21 na 23 mwaka huu
    wakati ya marudiano itakuwa nyumbani Oktoba 6 mwaka huu.
     
    Boniface Wambura
    Ofisa Habari
    Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
    Khartoum, Sudan
    Mei 3, 2012
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGORONGORO WATUA SALAMA KHARTOUM TAYARI KUMALIZA KAZI KESHOKUTWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top