![]() |
| Okwi akifanya vitu vyake |
HAMISI Kiiza ni mwanasoka bora wa Uganda kwa mwaka uliopita,
tuzo aliyopewa mwaka huu.
Huyu anatarajiwa kuwa mmoja wa watu watakaoongoza safu ya
ushambuliaji ya Yanga kwenye mechi ya Jumamosi dhidi ya watani wa jadi, Simba
SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kiiza au Diego, alisajiliwa Yanga msimu huu, baada ya kung’ara
akiwa na timu ya taifa ya Uganda chini ya umri wa miaka 23, The Kobs ambayo
iliitoa Tanzania katika kuwania tiketi ya kucheza Michezo ya Afrika (AAG) iliyofanyika
mwaka huu Maputo, Msumbiji.
Emmanuel Okwi ni mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uganda
ambaye alikuwemo kwenye kikosi cha The Cranes kilichotwaa Kombe la Challenge
Desemba mwaka jana mjini Dar es Salaam.
Huyu anatarajiwa kuwa miongoni mwa watu watakaoongoza safu
ya ushambuliaji ya Simba katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Yanga.
![]() |
| Kiiza akimtoa Nassor Masoud Chollo wa Simba kwenye mechi iliyopita |
Katika mchezo huo wa funga dimba Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, Waganda hao watakuwa na jukumu la kuonyeshana nani zaidi baina
yao- kwa kila mmoja kuhakikisha anaibeba timu yake.
Katika siku za karibuni, wachezaji hawa wote wawili wamekuwa
kwenye kiwango cha juu mno na wanafunga mabao mfululizo, tofauti ni kwamba Okwi
timu yake inaendelea kwenye mashindano ya Afrika.
Kiiza aliwafunga Zamalek, Yanga ikitoa sare ya 1-1 katika
Ligi ya Mabingwa Afrika, bahati mbaya timu yake ikatolewa, lakini Okwi
ameendelea kuibeba Simba kwa mabao yake kwenye Kombe la Shirikisho, bao muhimu
zaidi lile lililoitoa mashindanoni ES Setif mjini Setif, Algeria, Simba ikilala
3-1 na kufuzu kwa faida ya bao la ugenini, baada ya awali kushinda 2-0 Dar es
Salaam.
Katika Ligi Kuu, Yanga ilipoteza dira tu- lakini Kiiza
amekuwa akifunga karibu katika kila mechi kama ilivyo Okwi.
Okwi ana misimu mitatu Tanzania, lakini hajawahahi kuifunga
Yanga hata bao la offside, wakati Kiiza aliwafunga Simba Julai 10, mwaka jana
katika Fainali ya Kombe la Kagame, ingawa refa alikataa bao hilo akidai
aliotea.
Okwi ameshindwa kuifunga Yanga hadi kufikia kupoteza imani
mbele ya mashabiki wa Simba kwenye mechi za watani, kama hana madhara.
Ilifikia Okwi ikadaiwa alipigwa ‘mangumi’ na Haruna Moshi ‘Boban’
baada ya mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Yanga, Simba
ikilala 1-0, akishutumiwa kukosa mabao kizembe.
Wakati tunaingia kwenye mchezo wa watani wa jadi, watu
hawakumbuki tena historia ya Okwi na mechi za watani, zaidi ya kiwango chake kizuri
hivi sasa akiwa anaibeba mno Simba siku za karibuni.
Lakini wakiwa wanacheza Tanzania, kila mmoja anataka
nyumbani Uganda wajue yeye ni zaidi na pia kujitengenezea mazingira ya kuitwa
kwenye timu yao ya taifa, The Cranes.
Bobby Williamson, kocha Mscotland wa Uganda anaweza asiwafuatilie
wachezaji hao msimu wote wanafanya nini Tanzania, lakini katika mechi kama hizi
za watani wa jadi, lazima atataka kujua nani amefanya nini.
Zaidi Williamson ataangalia takwimu za mchezaji katika ligi
anayocheza kama kigezo cha kumuita timu ya taifa.
Wachezaji hawa wawili wote ni hatari na wana kiu ya kufunga.
Wote wana nafasi ya kupangwa Jumamosi kwa namna yoyote ile. Wawili hawa kwa
hakika ni sehemu ya chachandu za mpambano wa watani wa jadi Jumamosi.




.png)
0 comments:
Post a Comment