• HABARI MPYA

  Wednesday, June 07, 2017

  YOSSO WAMPA KIBURI MWAMBUSI YANGA, ASEMA WATATUMIA AKILI KUWANG'OA WAKENYA 'MIILI NYUMBA'

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  KOCHA wa Yanga, Juma Mwambusi amesema kwamba anafahamu kesho watakutana na timu yenye wachezaji wenye miili mikubwa, AFC Leopards ya Kenya, lakini watatumia maarifa kuwatoa.
  Yanga itamenyana na Leopards katika Nusu Fainali ya kwanza ya michuano ya SportPesa Super Cup kuanzia Saa 8:00 mchana Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Na ikiwa na wachezaji wengi vijana wadogo wa timu ya pili, baada ya wachezaji wake wengi wa kikosi cha kwanza kuchukuliwa na timu zao za taifa kwa mechi za kwanza za makundi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2019 wikiendi hii – Yanga haipewi nafasi ya kufurukuta mbele ya timu ya Kenya.
  Juma Mwambusi amesema kesho watatumia akili tu kuitoa AFC Leopards yenye wachezaji wenye miili mikubwa 

  Lakini kocha Msaidizi, Mwambusi anayeiongoza timu kwenye mashindano haya wakati bosi wake, Mzambia George Lwandamina amekwenda likizo nyumbani kwao amewatoa hofu wana Yanga katika mahojiano na Bin Zubeiry Sports - Online kuelekea mchezo huo.  
  Mwambusi amesema kwamba anatambua wapinzani wao hao wana wachezaji wenye vimo vikubwa na staili yao ya uchezaji ni mipira ya juu, lakini Yanga wamejipanga vizuri kukabiliana nao hiyo kesho kwa kucheza kiufundi zaidi.
  “Nina imani tutafanya vizuri, ikiwa Yanga ndiyo timu pekee ya Tanzania iliyobaki kwenye mashindano haya, hivyo vijana wangu watafanya vizuri na kushinda mechi ya kesho ili tuingie fainali inshaallah,”amesema Mwambusi.
  Nusu Fainali nyingine kesho itazikutanisha timu za Kenya tupu, Gor Mahia iliyoitoa Jang’ombe Boys ya Zanzibar jana kwa mabao 2-0 ya Meddie Kagera na Nakuru All Stars iliyoitoa Simba SC ya Dar es Salaam kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
  Vijana wadogo wa Yanga wakiongezewa nguvu na kaka zao wachache tu, akiwemo Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa kikosi cha Yanga, waliwastaajabisha watu juzi baada ya kuwazima mabingwa wa Kenya, Tusker FC kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0.   
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YOSSO WAMPA KIBURI MWAMBUSI YANGA, ASEMA WATATUMIA AKILI KUWANG'OA WAKENYA 'MIILI NYUMBA' Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top