• HABARI MPYA

    Saturday, June 10, 2017

    TFF YAOMBA MICHANGO ZAIDI KWA AJILI YA TIMU ZA TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limewaomba Watanzania kuendelea kuchangia Mfuko wa Maendeleo ya Soka (FDF), kwani bado wanakabiliwa na changamoto nyingi.
    Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas Mapunda amesema leo katika taarifa yake kwamba, shirikisho linakabiliwa na changamoto za mashindano mbalimbali kwa timu zote za taifa za wanawake na wanaume kuanzia za vijana hadi wakubwa.
    “Tunaomba michango iendelee kwani bado tuna changamoto za mashindano mbalimbali kwa timu za wanawake na vijana ikiwemo fainali za wanawake Afrika zitakazofanyika Ghana hapo mwakani kwa timu ya Twiga Stars na AFCON 2019 kwa Serengeti Boys ambayo itakuwa mwenyeji,”amesema.
    Pamoja na hayo, Mapunda amekana madai kwamba TFF imewatelekeza wachezaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys baada ya kurejea kutoika Gabon waliposhiriki Fainali za Afrika mwezi uliopita.
    “Madai kwamba eti (wachezaji wanalalamika) hawakulipwa posho na kushutumu viongozi wa juu wa shirikisho kuhusu jambo hilo. Hizi taarifa si za kweli. TFF inapenda kuwajulisha wazazi na umma kwa ujumla kwamba vijana wetu walilipwa posho zao zote wakiwa kambini Morocco na Cameroon na zile za mashindano ya AFCON nchini Gabon,”amesema Mapunda.
    Aidha, Ofisa huyo amesema shirikisho linafanya taratibu za kupeleka maombi FDF ili kupata fedha za kuwalipa vijana na benchi la ufundi sehemu ya posho walizokuwa hawajalipwa.
    “Tumeshtushwa na taarifa hizo ambazo tafsiri yake ni kuharibu uhusiano mwema kati ya shirikisho, wazazi na wachezaji ambao wanatarajiwa  kuitumikia timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka  20 maarufu kama Ngorongoro Heroes,”.
    “Shirikisho linaendelea kuwatambua vijana wa Serengeti Boys kwani bado ni sehemu ya kikosi cha Ngorongoro Heroes na hivyo ukifika wakati wataitwa kambini kwa ajili ya michezo ya kimataifa ya U-20.  TFF inazidi kuushukuru umma ambao umeendelea kuchangia Mfuko wa FDF ambao kimsingi kazi yake ni kutafuta rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya mpira,” amesema Mapunda.
    Mfuko wa Maendeleo ya Mpira - FDF ulianzishwa kwa lengo la kutafuta rasilimali za maendeleo ya mpira wa miguu hasa kwa wanawake na vijana pamoja na miundombinu ya mchezo huo.
    Mfuko huo uko chini ya Mwenyekiti, Tido Mhando anayeongoza Bodi na Mtendaji Mkuu wake ni Dereck Murusuri anayesimamia sekretarieti.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAOMBA MICHANGO ZAIDI KWA AJILI YA TIMU ZA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top