• HABARI MPYA

  Sunday, June 11, 2017

  MAYANGA KACHEMKA JANA, LAKINI APEWE MUDA

  WAKATI ratiba inatoka, Tanzania imepangwa Kundi L  kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon pamoja na Uganda, Cape Verde na Lesotho, ubashiri ulikuwa kundi jepesi. 
  Wachambuzi, wachezaji wa zamani na vyombo vya Habari kwa ujumla vilichukulia Kundi L kama njia nyepesi zaidi ya kurudi AFCON tangu mwaka 1980. 
  Lakini jana, Tanzania imetia mguu kwenye mchezo wake wa kwanza wa kundi hilo ‘mchekea’ na kulazimishwa sare na ‘vibonde’ Lesotho 1-1, nyumbani. 
  Maana yake, Stars imeanza vibaya mbio za kuwania tiketi ya Fainali za AFCON 2019 nchini Cameroon baada ya sare hiyo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Sare hiyo inamaanisha kocha Salum Mayanga ameshindwa kuvunja mwiko wa muda mrefu wa Taifa Stars kutoshinda mechi zaidi ya mbili, baada ya kushinda mechi mbili za kirafiki mwezi Machi 2-0 dhidi ya Botswana na 2-1 dhidi ya Burundi.
  Tanzania jana ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 27 kupitia kwa Nahodha wake, Mbwana Ally Samatta kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya beki wa kushoto, Gardiel Michael kuangushwa nje ya boksi.                        
  Hata hivyo, bao hilo halikudumu, kwani Lesotho, au Mamba walisawazisha dakika ya 34 kupitia kwa Thapelo Tale aliyeunganisha pasi nzuri ya Jane Thaba-Ntso.
  Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, timu zote zilishambuliana kwa zamu, lakini Lesotho ndiyo waliocheza vizuri zaidi kwa kuonana na kutawala sehemu ya kiungo.
  Na hiyo ilitokana na mfumo wa wenyeji kuweka mawinga wawili pembeni na washambuliaji wawili mbele, hivyo kujikuta inaelemewa sehemu ya katikati ya Uwanja ambako walikuwepo Himid Mao na Muzamil Yassin pekee.
  Kasi ya mashambulizi ya Stars iliongezeka mwishoni mwa mchezo baada ya mabadiliko yaliyofanywa mfululizo na Mayanga akiwatoa Thomas Ulimwengu, Simon Msuva na Muzamil Yassin na kuwaingiza Farid Mussa, Mbaraka Yussuf na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
  Na baada ya mechi, pengine kutokana na imani ya mapema ya kwamba Kundi L ni jepesi, kocha na wachezaji wamebebeshwa lawama.
  Mashabiki wanasema wachezaji wengi walicheza chini ya kiwango jana, hawakujituma na wengine wanaponda mbinu za kocha hususan katika upangaji wa timu.
  Wengine wanalaumu uamuzi wa kuupeleka mchezo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ulisababisha matokeo mabaya.
  Ikumbukwe mchezo huu umwefanyika Uwanja wa Azam kwa sababu Uwanja wa Taifa unafanyiwa ukarabati.  
  Nahodha Samatta alisema baada ya mechi kwamba udogo wa Uwanja wa Azam uliwakosesha ushindi dhidi ya Lesotho.
  Stars inayofundishwa na kocha Salum Mayanga, ilitangulia kwa bao la Samatta dakika ya 27 kwa shuti zuri la mpira wa adhabu, kabla ya Mamba kusawazisha kupitia kwa Thapelo Tale dakika  ya 34.
  “Uwanja wa azam Complex ni mdogo sana, kitu ambacho kwa upande wetu ambao wengi tumezoea kucheza Uwanja wa mkubwa wa Taifa  kimetufanya tujibane, tumeshindwa kucheza kwa uwezo wetu mechi ya leo, yaani ukipewa mpora ukigeuka, Uwanja umekwisha,”alisema.
  Samatta pia akalaani staili ya ukabaji wa mabeki wa Lesotho, akisema walikuwa wanamfuata watatu kwa wakati mmoja hadi kuna wakati akajikuta anakasirika.
  “Nimekasirishwa na kitendo cha kutoka sare na Lesotho, sijafurahishwa kabisa ukiangalia tumecheza nyumbani na haikuwa akilini mwangu kama matokeo yangekuwa hivi, lakini ndio imekuwa hivi, tunawaahidi Watanzania tutafanya vizuri katika mechi zijazo,”alisema.
  Kwa upande wake; Mayanga alisema watazinduka na kufanya vizuri katika mechi zijazo baada ya sare ya leo.
  Taifa Stars ilianza vibaya mbio za Cameroon 2019 usiku wa jana, baada ya kulazimishwa sare ya nyumbani 1-1 na Mamba wa Lesotho. 
  Mayanga pia alilaani kitendo cha safu yake ya ulinzi kuruhusu bao la kusawazisha la Lesotho lililofungwa Thapelo Tale dakika  ya 34, kufuatia Nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta kufunga la kuongoza dakika ya 27.
  “Tumefanya makosa kuruhusu goli rahisi la Lesotho, lakini sare ya leo haitukatishi tamaa na tutaendelea na mazoezi kama kawaida kwa ajili ya mechi zilizosalia. Naamini makosa ya  leo tutayafanyia kazi na tutazinduka, tutafanya vizuri,”amesema Mayanga. 
  Kocha huyo aliyerithi mikoba ya mzalendo mwenzake, Charles Boniface Mkwasa ameongeza kwamba Lesotho jana walikuwa wanatumia mbinu ambazo ni changamoto kwake na atazifanyia kazi.
  Mshambuliaji wa zamani wa Taifa Stars, Athumani Machuppa ameshauri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litafute kocha wa kiwango cha juu kwa ajili ya timu ya taifa, Taifa Stars, kwani Salum Mayanga peke yake hawezi. 
  “Kwani kuna ubabaishaji gani kutafuta kocha wa maana mwenye Cv za Kutosha....timu yetu haichezi kitimu, hatujui mashambulizi yaanzie wapi, kiongozi wetu pekee Mbwana Ally Samatta,”alisema.
  “Natamani kuona tunapata kocha mkubwa, ambaye atasaidiana na Mayanga, kikosi cha Stars cha mechi ya mwisho kilikuwa kizuri mno kiwango chao, lakini sielewi...nimebahatika kuangalia mechi kipindi kimoja cha mwisho, ila mapungufu ni mengi mno,”aliongeza.
  Machuppa aliyekuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichotwaa Kombe ka CECAFA Castle mwaka 2002 Mwanza, amesema kwamba kama Tanzania tuna mpango wa kwenda fainali za AFCON 2019 tuamke kabla jua halijakuchwa.
  Haya yote ni kwa sababu Taifa Stars ilicheza ovyo na haikupata ushindi jana.
  Kweli timu yetu ilicheza ovyo – kocha aliweka washambuliaji wa pembeni wawili na safu ya kiungo ikapwaya matokeo yake timu ikazidiwa.
  Hii ni changamoto kweli kwa kocha Mayanga, kwanza kuacha kupanga wachezaji kwa mazoea, na pili anahitaji kuwa na maamuzi ya haraka pale anapoona mipango aliyoingia nayo imefeli.
  Zaidi ya hapo, Mayanga apewe muda afanyie kazi mapungufu yaliyoonekana ili tuone mechi ijayo timu itarudi vipi. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAYANGA KACHEMKA JANA, LAKINI APEWE MUDA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top