• HABARI MPYA

    Tuesday, June 06, 2017

    JANG’OMBE BOYS WANG’OLEWA MAPEMAA SPORTPESA SUPER CUP

    Na Shekha Jamal, DAR ES SALAAM
    VIGOGO wa Kenya, Gor Mahia wamekwenda Nusu Fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Jang’ombe Boys ya Zanzibar mchana huu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Shukrani kwake, mfungaji wa mabao yote hayo mawili, mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere.
    Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika timu hizo zikiwa hazijafungana na kipindi cha pili, mshambuliaji wa zamani wa Mbale Heroes FC ya Uganda, ATRACO FC ya Rwanda, Kiyovu Sports, Mukura Victory, Police FC na Rayon Sports za Rwanda, Zarzis ya Tunisia na KF Tirana ya Albania, Medie Kagere akafunga mawili.
    Meddie Kagere (kushoto) akipiga mpira pembeni ya beki wa Jang'ombe Boys, Ibrahim Said (kulia) leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam

    Mganda huyo aliyechagua kuchezea timu ya taifa ya Rwanda, alifunga bao la kwanza dakika ya 64 kwa kichwa akimalizia krosi ya Muguna Kenneth na la pili kwa penalti dakika ya 84, baada ya beki wa Jang’ombe Boys kuunawa mpira.
    Gor Mahia sasa itakutana na mshindi wa mchezo wa pili unaoanza hivi sasa, kati ya Simba SC ya Dar es Salaam na Nakuru All Stars.
    Ikumbukwe jana, mabingwa wa Tanzania, Yanga SC waliwatoa kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 mabingwa wa Kenya, Tusker FC na AFC Leopards wakaitoa Singida United kwa penalti pia 5-4 baada ya sare ya 1-1.
    Maana yake, Yanga SC itakutana na mabingwa wa zamani wa Kenya, AFC Leoparda keshokutwa hapa hapa Uwanja wa Uhuru.    
    Kikosi cha Gor Mahia kilikuwa; Fredrick Odhiambo, Haroun Shakava, Wellington Ochieng, Innocent Wafula, Joach Onyango, Philemon Odhiambo, Francis Kahata/John Ndirangu dk85, Kenneth Mugana, Timoth Otieno/Anthony Mbugua dk67, Meddie Kagere/Amos Nondi dk85 na Mike Simiyu/George Odhiambo dk59.
    Jang'ombe Boys; Ruga Hasham, Said Ibrahim, Amour Firdaus, Chandika Ibrahim, Ally Sammad, Abdi Kassim ‘Babbi’, Abdallah Rashid/Ali Aboukabar dk79, Makame Khamis, Juma Hafidh, Ali Shekha na Abdallah Hussein.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JANG’OMBE BOYS WANG’OLEWA MAPEMAA SPORTPESA SUPER CUP Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top