• HABARI MPYA

  Monday, June 05, 2017

  AZAM FC WANAPASWA KUJITAFAKARI UPYA MAPEMA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  BAADA ya miaka mitano ya kuwa moja ya timu zinazofanya vizuri katika soka ya Tanzania, ikishindania mataji na nafasi za uwakilishi kwenye michuano ya Afrka, Azam FC imefikia azimio la kubadili mfumo wake wa uendeshaji.
  Chini ya Mtendaji Mkuu mpya wa masuala ya klabu, Abdul Mohammed aliyechukua nafasi ya Saad Kawemba, Azam FC inataka kufuta sifa ya kutumia fedha nyingi katika usajili, na badala yake kusajili kwa bajeti ndogo tu.
  Zaidi Azam FC chini ya Abdul Mohammed, imeazimia kuitolea macho akademi yake, kwa kuitumia kama mtambo wa kuzalisha vipaji vya kutumika kikosi cha kwanza baadaye.
  Sera hizo zimeanza kufanya kazi kwa kufuta utamaduni wa kutoa dau kubwa kwa wachezaji kusaini mikataba, baada ya kuwaruhusu kuondoka wachezaji wakubwa wa klabu hiyo waliomaliza mikataba yao na kutaka fedha nyingi ili wabaki.
  Kwenye mkumbo huo ameingia mshambuliaji tegemeo wa klabu na wa muda mrefu, tangu timu inapanda Ligi Kuu, John Raphael Bocco aliyekuwa Nahodha wa timu pia.
  Bocco amemaliza mkataba na katika mazungumzo yake na klabu juu ya kusaini mkataba mpya hawakufikia makubaliano, kutokana na kile kilichoelezwa mchezaji huyo kutaka fedha nyingi tofauti na sera mpya za Azam ya Abdul Mohammed.
  Tayari kuna tetesi, Bocco ataibukia kwa Wekundu Msimbazi, Simba SC msimu ujao – huku wachezaji wengine, akiwemo kipa Aishi Manula na beki Shomary Kapombe wakitajwa kuwa njiani kumfuata.
  Lakini pamoja na utambulisho wa sera mpya za kutotumia fedha nyingi kusajili, uongozi wa Azam umesema upo kwenye mazungumzo na wote, Manula na Kapombe wabaki baada ya kumaliza mikataba yao.
  Maana yake, Azam FC inaweza kutumia fedha nyingi nje ya utaratibu wao mpya ili tu kuwabakisha wawili hao, huku ikiwa imekubali kumpoteza mchezaji wake muhimu na wa kihistoria, Bocco.
  Inaaminika moja ya sifa za klabu kuitwa kubwa ni pamoja na kuwa na magwiji wake na wachezaji kama Bocco pamoja na wengine waliodumu kwenye klabu hiyo tangu inaibuka Ligi Kuu kama akina Himid Mao na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ndiyo baadaye watakuwa magwiji wa klabu kama watamalizia soka yao hapo na kuagwa vizuri.
  Lakini baada ya kuwa na timu kwa takriban miaka 10 akitoa mchango mkubwa kwenye kuipandisha Ligi Kuu na pia kuchangia mafanikio yake kwa kiasi kikubwa, Bocco anaachwa katika hali ya kawaida mno.
  Labda kuwe kuna kitu kingine, lakini si kusema sera mpya za kutosajili kwa fedha nyingi ndizo zinamuondoa Bocco kwa sababu ametaka dau kubwa la usajili – na wakati huo huo klabu inasema ipo kwenye mazungumzo na Manula na Kapombe ili wabaki.
  Manula alitokea kwenye akademi ya Azam na Kapombe alisajiliwa kutoka AS Cannes ya Ufaransa iliyomtoa Simba SC, lakini Bocco alipanda na Azam FC na tukubali uongozi wa Azam FC unajua unachokifanya.
  Mchezaji wa kihistora wa Azam FC, John Raphael Bocco 'Adebayor' (kulia) ameruhusiwa kuondoka baada ya kumaliza mkataba wake

  SERA ZA KUTOTUMIA FEDHA:
  Ipo imani inayoaminika kwamba klabu inayofanya vizuri na kushinda mataji ni ile inayowekeza kwa kutumia fedha nyingi kusajili wachezaji wa kiwango cha juu.
  Taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya limedumu Hispania na hiyo ni kutokana na sera za klabu kubwa za huko, Barcelona na Real Madrid kutoa fedha nyingi kusajili wachezaji bora.
  PSG na Monaco za Ufaransa zimeanza kutema cheche tena kwenye michuano ya Ulaya baada ya wawekezaji wapya kuja kuziinua kiuchumi na kuzifanya zisajili wachezaji wakubwa.
  Hata kwenye Ligi Kuu mbalimbali, timu zinazofanya vizuri ni zile ambazo ukitazama vikosi vyake utagundua kuna wachezaji wa gharama kubwa.
  Hakuna ubishi mkubwa juu ya sera ya kutumia fedha nyingi katika timu ili kuwa na kikosi imara cha ushindani pamoja na kuwepo na mifano ya timu ambazo zilifanikiwa pasipo kutumia fedha nyingi sana kama Leicester City.
  Kwa sababu hii, tuseme sera mpya ya Azam FC kutotumia fedha nyingi kusajili maana yake inawaondoa kwenye orodha ya timu zinazoshindania mataji?
  Bila shaka – katika wakati ambao inaibuka timu kama Singida United, inayotumia fedha nyingi kusajili wachezaji wazuri na huku timu kama Kagera Sugar na Mtibwa Sugar zikizidi kuimarika, wazi Azam FC inajiweka pagumu kwa sera zake mpya inazotaka kuja nazo.  
  Farid Mussa (kulia) ambaye kwa sasa anacheza Hispania ni moja ya matunda ya akademi ya Azam FC

  KUPANDISHA WACHEZAJI WA AKADEMI
  Moja ya klabu ambazo inaaminika zina mifumo imara ya soka ya vijana ni Barcelona na La Masia yake, ambayo imemtoa mwanasoka bora kabisa wa kizazi hiki, Lionel Messi.
  Lakini bado Barcelona hiyo hiyo imetoa mamilioni ya Euro kusajili nyota kutoka sehemu nyingine, wakiwemo Luis Suarez na Neymar Junior.
  Azam ina akademi imara nzuri na ambayo ilisifiwa hadi na Mwanasoka Bora wa zamani Afrika, Abedi Pele alipozuru nchini na kufika hadi Chamazi Novemba mwaka 2012, lakini bado kama klabu inataka kushindani mataji, haiwezi kukwepa kununua wachezaji nje ya mfumo wake wa soka ya vijana.
  Kwani ukitazama vikosi vya Azam kwa misimu yote mitano iliyopita, wachezaji waliopandishwa kutoka akademi wamekuwa hawakosekani na miongoini mwao wapo kwenye kikosi cha sasa akina Manula, Gardiel Michael, Mudathir Yahya, Shaaban Iddi na Masoud ‘Cabaye’ Abdallah.
  Farid Mussa baada ya kufanya vizuri Azam FC kufuatia kupandishwa kutoka akademi, kwa sasa anacheza timu ya Daraja la Kwanza Hispania, DC Tenerife.
  Kwa hivyo Azam FC kupandisha wachezaji wa akademi imekuwa sera ya klabu kwa muda mrefu na si sera mpya inayokuja sasa chini ya uongozi wa Abdul Mohammed.
  Isipokuwa uongozi wa Abdul Mohammed baada ya msimu mmoja wa kutumia fedha nyingi, tena za rekodi sasa unaamua kujishusha kwa kasi baada ya kuona umeitia hasara kubwa klabu na matokeo ya msimu hayakuwa mazuri.
  Kutoka benchi la Ufundi la Waspaniola watupu mwanzoni mwa msimu na kuachwa kwa wachezaji wote wa kigeni waliokuwapo wa Ivory Coast, Serge Wawa, Kipre Balou na Ya Thomas Lenardo, Mzimbabwe, Francesco Zekumbawira, Mrundi Didier Kavumbangu, Mkenya Allan Wanga na Mnyarwanda Jean Baptiste Mugiraneza hakika fedha nyingi ‘zilichomwa moto’.
  Na hata baada ya kusajiliwa Waghana Yakubu Mohammed, Daniel Amoah, Yahya Mohammed, Enock Atta Agyei, Samuel Afful na Mcameroon Stephan Mpondo kwa mamilioni ya fedha, bado mambo hayaendi vizuri ndipo maamuzi magumu yanafikiwa bila kujali athari zake.
  Benchi la Ufundi la Azam FC kutoka kulia, Kocha Mkuu Mromania, Aristica Cioaba na wasaidizi wake, Iddi Cheche, Meneja Philipo Alando na kocha wa makipa, Iddi Abubakar

  NINI AZAM ILIPASWA KUFANYA BAADA YA MSIMU?
  Baada ya msimu mbaya zaidi ndani ya miaka mitano, Azam FC ilipaswa kuwa na kikao cha tathmini ya kina na kirefu, hatua kwa hatu kikihusisha idara zote kujaribu kutazama wapi walipokosea.
  Kutoka makocha wa Hispania hadi kocha Mromania, Aristica Cioaba na wachezaji wote waliosajiliwa na kuachwa ambao hakika ni wazuri, inakuwjae timu inamaliza msimu vibaya?
  Katika soka kuna mambo mengi zaidi ya kusajili wachezaji wazuri, wakati mwingine aina ya matayarisho kuelekea mechi, huduma kwa wachezaji, nidhamu na hata falsafa za kocha husababisha timu isifanye vizuri.
  Je, kipi kilikuwa tatizo ndani ya Azam FC na hata maamuzi yawe ya kivivu tu kwamba timu iache kutumia fedha nyingi kusajili.
  Inaonekana kweli kumekuwa na matumizi mabaya ya fedha ndani ya Azam FC na ambayo pengine yanaweza kuwa yamewafikisha hapa wamiliki wake, kuona kuendelea kutumia fedha nyingi ni kuzidi kujitia hasara.
  Baada ya kuwa na akademi, Azam FC inaweza kusajili kila baada ya angalau miaka mitatu hadi mitano, kama ambavyo unaweza kuona Barcelona inafanya – lakini kwa timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake mambo ni tofauti, imekuwa ikisajili kila dirisha, tena ikiacha karibu wote na kusajili karibu wapya wote hususan wa kigeni.  
  Azam FC inapaswa kufikiria upya uamuzi wake, kwani sera za kutotumia fedha kusajili zinaweza kuiondoa timu moja kwa moja kwenye ushindani wa mataji na kuwa timu mfano wa Mtibwa Sugar ambayo haina malengo ya mataji tena zaidi ya kuwepo tu. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC WANAPASWA KUJITAFAKARI UPYA MAPEMA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top