• HABARI MPYA

    Tuesday, December 04, 2012

    KIIZA, OKWI KUJILENGESHA AU KUJIKWEPESHA KWA STARS LEO?

    Kikosi cha Uganda, Okwi wa kwanza kulia waliosimama na Kiiza ameinama mbele yake

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    ROBO Fainali za mwisho za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge zinatarajiwa kupigwa leo kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa.
    Kenya, mabingwa mara tano wa Kombe hilo katika miaka ya 1975, 1981, 1982, 1983 na 2002, watamenyana na Malawi walioalikwa tu kuongeza changamoto ya mashindano kuanzia saa 10:00 jioni.
    Wenyeji, mabingwa watetezi na mabingwa wa kihistoria wa mashindano haya, Uganda The Cranes waliotwaa Kombe hilo katika miaka ya 1973, 1976, 1977, 1989, 1990, 1992, 1996, 2000, 2003, 2008, 2009 na 2011, watamenyana na Ethiopia.
    Ethiopia ni timu pekee kati ya wanachama wa CECAFA, iliyofuzu kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Afrika Kusini.
    Mchezo kati ya Kenya na Malawi unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua hata kama mashabiki hawatakuwa wengi uwanjani.
    Kenya na Malawi ni vigumu kuutabiri kulingana na viwango vilivyoonyeshwa na timu zote katika mashindano haya kutopishana sana.
    Lakini Uganda wanapewa nafasi kubwa ya kuwafunga Ethiopia, ambao katika michuano hii hawajaonyesha kiwango cha kutisha kama ilivyo kawaida yao licha ya kufuzu AFCON.
    Brian Umony, Hamisi Kiiza, Rpbert Ssentongo na Emmanuel Okwi- hizi zinatarajiwa kuwa silaha za Korongo wa Kampala katika mchezo wa leo, lakini pia yupo kiungo mmoja hodari sana Joseph Oyola.  
    Katika Robo Fainali za kwanza jana Uwanja wa Lugogo, Zanzibar iliichapa Burundi kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90. Kwa matokeo hayo, Zanzibar sasa itacheza na mshindi kati ya Kenya na Malawi katika Nusu Fainali.
    Shujaa wa Zanzibar jana alikuwa ni Abdallah Othman aliyefunga penalti ya mwisho, baada ya kipa Mwadini Ally kupangua penalti ya Abdul Fiston wa Burundi.
    Manahodha wa timu zote, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Zanzibar na Suleiman Ndikumana wa Burundin walipoteza penalti zao jana.
    Ndikumana alikuwa wa kwanza kwenda kupiga na mkwaju wake ukaota mbawa na kupaa juu ya lango, wakati wenzake waliofunga mbali na Fiston kupoteza ni Steve Nzigamasabo, Amisi Tambwe, Chris Nduwarugira, Leopold Nkurinkiye na Gael Duhatindavyi.
    Upande wa Zanzibar Heroes, Khamis Mcha ‘Vialli’ alikwenda kufunga penalti ya kwanza ya Zanzibar, Adeyom Saleh Mohamed akafunga ya pili, Jaku Juma akafunga ya tatu, kabla ya Cannavaro kumpelekea mikononi mkwaju wake kipa Arthur Arakaza wa Burundi, Samir Hajji Nuhu akafunga ya tano, Aggrey Morris akafunga ya sita na Othman kutumbukiza nyavuni ya ushindi.
    Mapema katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali, Bara ilifanikiwa pia kuingia Nusu baada ya kuilaza Rwanda mabao 2-0 kwenye Uwanja huo huo wa Lugogo mjini hapa.
    Hadi mapumziko, Stars walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba, dakika mya 33 akiunganisha pasi ya Mwinyi Kazimoto aliyewapunguza wachezaji wawili wa Rwanda kabla ya kutoa pasi maridadi.
    Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Mohamed El Fadil kutoka Sudan, mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Rwanda na aliwafanya waende kwenye vyumba vya kupumzikia wakiwa hoi.
    Katika hicho kipindi cha kwanza, Rwanda walikosa bao la wazi dakika ya 12 baada ya krosi ya Jean Claude Iranzi kuokolewa na beki Kevin Yondan kwa kichwa na dakika ya 19 Jean Baptiste Mugiraneza alipiga juu akiwa nje kidogo ya eneo la hatari.
    Stars pamoja na kufunga bao hilo kipindi hicho cha kwanza, katika dakika ya 30 krosi nzuri ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa na Bocco walishindwa kuiunganisha na ikawapita wote.
    Ngassa tena, katika dakika ya 38 alipiga shuti kali kutoka wingi ya kushoto, lakini likaenda nje sentimita chache.
    Kipindi cha pili Stars walirudi vizuri tena na kuendelea kucheza kwa kuonana, ingawa na Rwanda nao waliendelea kucheza kwa bidii kutafuta bao la kusawazisha.
    Hata hivyo, walikuwa ni Stars tena waliofanikiwa kupata bao la pili dakika ya 53 baada ya John Bocco kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Jean Claude Ndoli kufuatia shuti kali la Mwinyi Kazimoto kutoka nje ya eneo la hatari.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KIIZA, OKWI KUJILENGESHA AU KUJIKWEPESHA KWA STARS LEO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top