• HABARI MPYA

    Tuesday, May 08, 2012

    RUSHWA INAUA SOKA LA TANZANIA- STEWART HALL



    SAMSON MFALILA, Gazeti la Mwanaspoti 
    KOCHA wa Azam, Stewart Hall amelia na wadau wa Simba na Yanga wanavyoipiga vita timu yake, ambayo imeibuka kuwa kigogo cha Ligi Kuu Tanzania Bara.

    Akizungumza na Mwanaposti katika mahojiano maalumu, Hall anasema anashangazwa na mashabiki hasa wa Simba na Yanga kwa kuijengea chuki timu yake kutokana na kutishia ubabe wao.

    Hall anaonya kuwa tabia ya wadau wa Simba na Yanga wanaotaka kuona ligi ya Tanzania ikitawaliwa na timu mbili zao tu kitu ambacho si sahihi kwa maendeleo ya soka.

    "Timu hizi zimekuwepo kwa miaka mingi sana lakini nashangaa zimeshindwa kusaidia kukuza soka la Tanzania.

    "Ninachokiona katika soka la Tanzania kinanisikitisha na kinachonikera zaidi wameingia watu makini wa Azam, ambao wameingiza fedha lakini wanapigwa vita," anasema Hall, ambaye ni raia wa Uingereza.

    Anasema Watanzania wanapaswa kuruhusu ushindani na kutolea mfano Ligi Kuu Scotland inavyoshindaniwa na timu mbili tu za Rangers na Celtic na kufanya soka la sehemu hiyo kuwa chini.

    Ligi Kuu Tanzania Bara
    Hall anasema anafurahia timu yake kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa miaka chache tangu kuanzishwa kwake.

    Anaeleza ni kitu kizuri kuona timu yake iliyoanzishwa mwaka 2004, imeipiku Yanga iliyoasisiwa katika miaka ya 1930.

    Azam safari hii imenyakua nafasi ya pili na mwakani itashiriki katika mashindano ya Kombe la Shirikisho.

    Hall anaonya Watanzania wanapaswa kubadilika kama kweli wanataka soka la nchi hii ibadilike.
    Anasema kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linatakiwa kuwa makini katika kuendesha katika ligi hiyo.

    Analalamikia vitendo vya rushwa kwenye ligi hiyo na viwango duni vya uchezeshaji miongoni mwa waamuzi.

    Hall anaeleza kuwa anashangaa kuona rushwa na upangaji matokeo vinakubalika kama sehemu ya soka la Tanzania.

    "Ni hatari kwa soka la nchi yenu kama mtakubali masuala ya upangaji matokeo," anasema Hall, ambaye timu yake ililazimika kurudiana na Mtibwa kwenye mzunguko wa pili baada ya mechi ya kwanza kukatizwa kutokana na makosa ya mwamuzi Rashid Msangi.

    Pia mechi za Yanga na Polisi Dodoma zilimalizika kwa waamuzi kupigwa kutokana na timu hizo kudai mwamuzi alikuwa anaibeba Azam.

    Kocha huyo anakanusha vikali madai hayo na kudai kuwa watu wanaionea wivu tu timu yake kutokana na kuwa na fedha nyingi.

    Hall anasema TFF kwa kushirikiana na wadau wa soka la Tanzania wanapaswa kupiga vita kwa nguvu zote masuala ya rushwa.

    Anatahadharisha ni ndoto kwa timu za Tanzania kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa kama wadau wa soka watakumbatia rushwa kama sehemu ya soka la Tanzania.

    Anasema wapangaji matokeo wanapaswa kuchukua hatua kali kama Marseille ya Ufaransa ilivyoadhibiwa mwaka 1993 baada ya kubainika ilikuwa inanunua baadhi ya mechi za Ligi Kuu Ufaransa au ile kashfa ya upangaji matokeo ya Italia iliyokuja kujulikana kwa jina la Calciopoli.

    Anaonyesha kuwa ubaya wa timu kununua mechi unasababisha Tanzania kuwakilishwa na timu dhaifu kwenye michuano ya Afrika.

    "Bwana mwandishi jiulize, timu gani ya Tanzania imetwaa kutwaa taji la Afrika? Jibu linafahamika na ni wazi kuwa linasababishwa na rushwa ndani ya Ligi Kuu," anaeleza Hall, ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Birmingham.

    Hall, hata hivyo, anadai anategemea ushindani mkali zaidi msimu ujao kwenye Ligi Kuu kwani ameona timu kama Mtibwa na Coastal Union ziko juu.

    Mashabiki wa Simba na Yanga
    Hall anaeleza pia mashabiki wa Simba na Yanga kwa kiasi kikubwa nao wanachangia kwa kiasi kikubwa kuvuruga soka la Tanzania.

    Anasema mashabiki hao wanaweka presha kubwa kwa wachezaji na viongozi wa soka kuhakikisha timu zao zinashinda.

    Hall anatolea mfano vurugu za mechi ya Yanga na Azam kuwa zilichangiwa zaidi na viongozi na mashabiki wa Yanga kuwapa shinikizo wachezaji wao kushinda.

    "Unajua tulikuwa tumeifunga Yanga mara kadhaa, sasa safari hii wakaona hapana wanapaswa kushinda kwa njia zozote. Basi baada ya kuona mambo hayaendi vizuri wakampiga mwamuzi," anasema Hall, ambaye pia ni Mshauri wa Ufundi wa timu ya Zanzibar.

    Hall anasema anaelewa mashabiki wa soka wa Tanzania wamegawanyika kushabikia timu hizo lakini amesema zinapaswa kubadilika.

    Anaeleza mashabiki wa timu hizo wanapaswa kuhakikisha timu zao zinaendeshwa kisasa zaidi ndani na nje ya uwanja badala ya kuendekeza siasa za nje ya uwanja.

    Hall anaeleza kutokana na presha na wingi wa mashabiki wa Simba na Yanga kumefanya wababaike wanapochezesha mechi za baina ya timu hizo.

    Pia ameponda mashabiki hao kwa kukosa uzalendo na kuzishabikia timu za kigeni zinapokuja kucheza Tanzania.

    "Nimefundisha soka katika nchi mbalimbali duniani lakini sijawahi kuona timu ya kigeni inashabikiwa," anasema Hall.

    Katika miaka ya karibuni, imekuwa kitu cha kawaida kwa mashabiki wa Simba na Yanga kushangilia timu za kigeni zinapocheza na mahasimu wao.

    Hall anasema ameshangazwa kuwa tabia hiyo imeingia katika timu ya taifa.
    "Mashabiki wa Simba na Yanga wanaua soka lenu kwani wameingiza siasa zao kwenye timu ya taifa," anaeleza Hall, ambaye alikuwa anazungumzia vituko vya Kombe la Chalenji mwaka jana wakati mashabiki wa Yanga walipokuwa wanaizomea timu ya Bara kutokana na kuwa na wachezaji wachache wa Yanga.

    Pia anatolea mfano jinsi mashabiki hao walivyokuwa wanamsakama mshambuliaji wake John Boko na kumfanya ajitoe kwenye kikosi cha timu ya taifa.

    "Boko ni mchezaji mdogo sana lakini ameacha kuchezea Stars kutokana na kujengewa chuki na mashabiki hawa. Watu hawa wanaua soka la Tanzania," anaeleza Hall.

    Pia anaeleza kuwa mashabiki hao wamejenga chuki kubwa dhidi ya timu yake kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na matajiri wa timu hiyo.

    Azam imejenga uwanja na hosteli ya wachezaji na ina mfumo mzuri wa timu kuanzia watoto wenye umri wa miaka 12.

    Pia wachezaji wa timu hiyo wanaangaliwa vizuri kwa kulipwa mishahara na marupurupu kwa wakati.

    "Mimi nilitegemea kuwa mashabiki hawa wangetuunga mkono na kushinikiza viongozi wao kubadilika na kuendesha timu zao vizuri lakini badala yake wanatupiga vita," anaeleza Hall kwa mshangao.

    Hall anatoa mwito kwa wadau wa soka la Tanzania kuiangalia Azam kama kioo cha soka la Tanzania badala ya kuichukulia kama adui.

    Maendeleo ya Azam
    Hall anaeleza kuwa anasema licha ya changamoto za waamuzi lakini anapongeza timu yake kwa kushika nafasi ya pili nyuma ya Simba iliyotwaa ubingwa.

    Amesema amefurahia kuona malengo yao yametimia msimu kwani walikuwa wanataka kuvunja ubabe wa Simba na Yanga kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

    "Lengo letu kubwa lilikuwa kushika nafasi mbili za juu, kitu ambacho tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

    "Sasa msimu ujao tunataka kupigania ubingwa jambo ambalo ninaamini tuna ubavu nalo," aliongeza Hall, ambaye amewahi kuzifundisha timu za taifa za St.Vincent, Grenada na Pune ya India.

    Hall anafichua kuwa timu hiyo imeandaa programu ya miaka 10 yenye lengo la kuifanya timu hiyo kuwa miongoni mwa timu kubwa Afrika.

    "Tunataka tufikie hatua kutoa upinzani kwa timu kama TP Mazembe au Al-Ahly ya Misri," anaongeza Hall.

    Amesema kuwa anasikitishwa na kuona timu yake inapigwa vita na wadau wa soka.
    Hall anasema kutokana na haya yanayowakuta Azam yatafanya watu wengine wenye fedha kuogopa kuingiza fedha zao kwenye soka.

    "Unajua kuna watu wanaangalia tunayofanya sasa watu wenye fedha zao wakishuhudia jinsi Azam inavyonyanyasika basi hawatataka kushiriki katika mchezo huu," anasema Hall, ambaye anaongeza fedha ni muhimu kwa maendeleo ya soka.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RUSHWA INAUA SOKA LA TANZANIA- STEWART HALL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top