Moja ya mechi zilizoikutanisha City na United msimu huu |
MSIMU huu wa Ligi Kuu ya England,
unatarajiwa kufungwa Jumapili, huku macho ya wengi yakiwa kwenye mechi mbili
zinazozihusu timu mbili kutoka Jiji moja, Manchester.
Timu hizo, Manchester City na Manchester United,
mojawapo itatawazwa kuwa bingwa Jumapili- lakini City wanapewa nafasi kubwa
zaidi.
Zikiwa zinalingana kwa pointi, City
inajivunia hazina yake kubwa ya mabao, ikiwa inaizidi mabao nane United.
City itamalizia nyumbani na QPR, ambayo
inapigana kuepuka kushuka daraja wakati United itamaliza na Sunderland.
Mark Hughes na kikosi chake wameahidiwa
pauni Milioni 1 na mmliki wa klabu hiyo, iwapo wataifunga au japo kutoka sare
na City.
Hughes alikuwa kocha wa City, kabla ya
kufukuzwa na nafasi yake kupewa Roberto Mancini- na watu sasa wanasubiri kuona
kama atalipa kisasi cha kufutwa kazi ‘kinyama’?
Sahau kuhusu hayo- ana kibarua cha
kuinusuru timu yake kushuka daraja, maana yake mechi hiyo kila timu itapigana
kufa na kupona, City ikiwania ubingwa na QPR ikitaka kubaki Ligi Kuu.
Tayati Sir Alex Ferguson amekwishakata tamaa,
akisema City inachukua ubingwa, hali ambayo ni tofauti na wiki tatu zilizopita,
wakati United lipokuwa ikipewa nafasi kubwa kabla ya kuteleza na kuiachia tena
City kupaa juu.
Msimu huu wa Ligi Kuu unakaribia kufanana
na msimu wa 2009/2010 ambao bingwa alipatikana katika mechi ya mwisho, United
tena wakipigana na Chelsea.
Chelsea iliizidi pointi moja tu United (86-85),
lakini hadi timu hizo zinaingia kwenye mechi za mwisho Mei 9, 2010 zilikuwa
zinalingana kwa wastani wa mabao (GD 24).
Chelsea iliifunga 8-0 nyumbani Wigan na
United ilishinda nyumbani pia 4-0 dhidi ya Stoke City.
United walikuwa wanaiombea Chelsea
ilazimishwe sare na Wigan na wao waifunge Stoke- lakini duwa la kuku
halikumpata mwewe na hapana shaka kwa kukumbuka hilo, sasa Ferguson amekubali kupokea
Medali ya Fedha.
Yatokee maajabu, labda City ipate ushindi
mwembamba wa 1-0 na ili United iwe bingwa inahitaji kushinda 10-0 dhidi ya
Sunderland.
Haitakuwa ajabu kwa United kupata ushindi
huo mnono, ikiwa msimu huu iliifunga mabao nane timu bora katika ligi hiyo,
Arsenal.
Lakini pia katika soka timu au wachezaji hujituma
kulingana na mahitaji- kama suala ni ushindi tu timu inaweza kuridhika baada ya
kutikisa nyavu za wapinzani mara mbili au tatu.
Lakini kama suala ni idadi ya mabao,
tumeshuhudia mara kadhaa timu zikipigania hilo na bila kwenda mbali hata hapa
Tanzania ishatokea, Simba iliwahi kufungwa 4-0 nyumbani na Mufurila Wanderers
ya Zambia, ikaenda kushinda 5-0 ugenini mwaka 1978- au Arsenal na AC Milan
katika Ligi ya Mabingwa msimu huu.
Ligi ya England ni tamu na itazidi
kujikusanyia wapenzi kutokana na upinzani wake- kwani katika wakati huu ambao
tayari La Liga, Bundesliga, Serie A zimekwishapata mabingwa wake- England mambo
yote yatajulikana baada ya kipyenga cha mwisho cha msimu.
ZILIVYOMALIZA CHELSEA NA UNITED 2009/2010:
P W D L GD Pts
1.Chelsea 38 27 5 6 32 86
2.Manchester United 38 27 4 7 28 85
ZINAVYOKABANA MSIMU HUU CITY NA UNITED
P
W D
L GD
Pts
1 Man City 37
27 5
5 63
86
2 Man Utd 37
27 5
5 55
86
Tathmini hii imeandikwa na Mahmoud Zubeiry
wa BIN ZUBEIRY blog usiku huu.
0 comments:
Post a Comment