Na Princess Asia
UCHAGUZI wa
viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake Tanzania (TWFA) unatarajia
kufanyika Desemba 19 mwaka huu mjini Morogoro.
Kwa mujibu
wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TWFA, Ombeni Zavala, uchaguzi huo
utatanguliwa na Mkutano Mkuu wa TWFA. Wajumbe wapiga kura wote wa mikoa
iliyofanya uchaguzi wake na kutoa taarifa za uchaguzi wao ofisi za TWFA
wanatakiwa kufika Morogoro siku moja kabla (Desemba 18 mwaka huu).
Wagombea
waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ni kama ifuatavyo;
wanaowania uenyekiti ni Isabela Kapera, Joan Minja na Lina Kessy. Rose Kissiwa
ni mgombea pekee wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Wanaowania
ukatibu mkuu ni Amina Karuma na Cecilia Mkafu. Nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inagombewa na Zena Chande pekee
baada ya Furaha Francis kujitoa kutokana na sababu za kifamilia.
Sophia
Charles na Triphonia Temba wanawania nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya
chama hicho.
Wagombea
Rahim Maguza, Macky Mhango na Rose Msamila wameondolewa kwa kushindwa kikidhi
matakwa ya Katiba ya TWFA Ibara ya 28(2).